Balozi wa Pakistan Saqlain Syedah apongeza ushirikiano kati ya Kenya na Pakistan

Balozi wa Pakistan hapa nchini Saqlain Syedah amepongeza uhusiano mwema uliopo kati ya Kenya na Pakistan hasa katika upande wa biashara na uwekezaji.

Amesema kuwa kwa sasa Kenya inauza asilimia 43 ya majani chai yake nchini Pakistan. Kwa upande wake Pakistan imetaja mchele kama bidhaa inayouzwa kwa wingi zaidi nchini Kenya.

“Kenya na Pakistan zimekuwa na uhusiano mwema tangu nyakazi za kabla uhuru. Asilimia 43 ya majani chai ya Kenya yanauzwa Pakistan ambako takribani asilimia 87 ya wananchi wanatumia bidhaa hiyo,” ameeleza.

Syedah ameyasema haya katika ukumbi wa mji wa Malindi, Kaunti ya Kilifi alipokutana na wakuu wa Bodi ya Manispaa ya Malindi pamoja na wale wa Chama cha Kitaifa cha Biashara na Viwanda, tawi la Kilifi.

Syedah amesema kuwa japo Pakistan inapokea majani chai kutoka nchi zengine bila kutozwa ushuru, nchi hiyo imeendelea kuagiza bidhaa hiyo kutoka Kenya, akidokeza kuwa kiasi cha mauzo ya majani chai kwa Pakistan kimeongezeka kutoka asilimia 41 mwaka uliopita hadi 43 mwaka huu.

“Japo tunapata majani chai bila ushuru kutoka sehemu zengine, tumesalia kuagiza kutoka Kenya. Kila mwaka, kiasi cha mauzo hayo kinaongezeka. Mwaka uliopita kilikuwa asilimia 41 na sasa ni 43,” amesema Syedah.

Ameongeza kuwa nchi hizo mbili ziko katika mazungumzo ya kufanya usawa wa kibiashara kwa kuwa sasa umeegemea sana upande wa Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *