Balozi wa Marekani ashtumu hatua ya kutumia vijana kuzua vurugu humu nchini

Balozi wa Marekani humu nchini Kyle McCarter amesema nchi yake haitabakia kimya na kutazama vijana wakiendelea kuchochewa na wanasiasa kuzua vurugu humu nchini.

Wakati uo huo, Kyle amekanusha madai kwamba nchi yake inapanga kufutilia mbali hati za Visa za maafisa wa ngazi za juu serikalini, kwa kukatiza uhuru wa kujieleza, kutangamana na kujikusanya pamoja humu nchini.

Balozi huyo ambaye alikuwa akiongea wakati wa ziara ya kutoa mchango wa barakoa kwa utawala wa Kaunti ya Kirinyaga, amesema hafahamu lolote kuhusu habari hizo huku akitaja madai hayo kuwa ya uongo.

Akiwa ameandamana na Gavana wa Kirinyaga Ann Mumbi Waiguru, Kyle pasipo kutoa maelezo zaidi amesema hakuna uamuzi wowote kama huo ambao umeafikiwa na nchi yake, na akahimiza WaKenya kupuuza uvumi wa aina hiyo.

Pia amesema kwamba wale watakaopatikana na hatia kufuatia kupotea kwa fedha za kupambana na janga la COVID-19, watakabiliwa na hatua kali kutoka kwa serikali yake.

Kuhusu usalama, Kyle amesema kwamba serikali za Marekani na Kenya zinashirikiana kwa karibu ili kushinda kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *