Baadhi ya wanawake wakataa BBI

Kundi moja la wanawake limepinga marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano wa BBI.

Kundi hilo limesema marekebisho ya katiba yatahujumu ufanisi ambao umeafikiwa na wanawake kufuatia katiba ya mwaka wa 2010.

Wanawake hao wamedai kwamba marekebisho hayo yanatumiwa kuwafumba macho wanawake kwani hayaelezei jinsi suala la jinsia litakavyoshughulikiwa kwenye Bunge la Kitaifa.

Wakiongozwa na Daisy Amdany, wanawake hao wamesema watahamasisha wanawake wengine na Wakenya kwa jumla kupinga mswada wa marekebisho ya katiba kupitia BBI.

“Ningependa kuomba akina mama wote wa Kenya tusimame pamoja tukatae BBI,” amesema mwanaharakati huyo.

Wamekashifu vikali mpango huo, wakihoji kuwa unanuiwa kuhujumu haki za kikatiba na uhuru wa wanawake.

Wamesema pendekezo la kuhakikisha uwakilishi sawa wa jinsia katika Bunge la Seneti ni hatua ya kuwafumba macho wanawake kwani watanyimwa fursa ya kuingia kwenye Bunge la Kitaifa ambalo litahusisha serikali pana.

Aidha wanawake hao wameisifu Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI, kwa kuanzisha uchunguzi kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007.

Wamehimiza idara hiyo kutumia mifumo ya jumla kushughulikia maovu yaliyotekelezwa hapa nchini bila kushawishiwa kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *