Categories
Habari

Kaunti ya Kirinyaga yajizatiti kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu

Serikali ya kaunti ya Kirinyaga imeimarisha juhudi za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu unaoendelea kuenea miongoni mwa wakazi wa kaunti hiyo.

Takwimu za idara ya afya ya kaunti hiyo zinaonyesha kwamba kaunti hiyo ina visa vingi vya ugonjwa wa kifua kikuu, ambapo watu 245 kati ya laki-1 walikuwa na ugonjwa huo kufikia mwaka 2018.

Visa vya ugonjwa huo kutoweza kuponywa na dawa viliongezeka kwa asilimia 50 kati mwaka   2016 na 2018, hali ambayo imetokana na kutozingatiwa vyema kwa maagizo ya utumizi wa dawa.

Gavana Anne Waiguru amesema kwamba idara ya afya imekuwa ikiwahamasisha wahudumu wa afya na wale wa kijamii ambao kisha huelimisha wananchi kuhusu kuzuia ugonjwa wa kifua kikuu, kupimwa kwa wakati ufaao na kutafuta huduma za matibabu.

Waiguru alisema serikali ya kaunti hiyo imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuwatenga na kuwatibu wagonjwa wa kifua kikuu kilicho na vitanda 24 katika hospitali ya Kerugoya.

‘Kituo hicho cha kuwatenga wagonjwa wa kifua kikuu kitasaidia katika uangalizi na pia  kuwatibu wagonjwa wa kifua kikuu,”alisema Waiguru.

Kwa upande wake waziri wa afya wa kaunti hiyo Gladys Kimingi alisema wagonjwa wa kifua kikuu wamekuwa wakipokea matibabu yanayofaa licha ya kuwepo kwa janga la Covid-19.

Alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo walio na dalili za kifua kikuu  zinazojumuisha kukohoa kwa muda mrefu kutembelea kituo hicho ili wapimwe na pia kupokea matibabu.

Categories
Habari

Shule moja yafungwa kaunti ya Kitui kutokana na maambukizi ya Covid-19

Shule nyingine imefungwa katika kaunti ya Kitui baada ya mwalimu mmoja kuthibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Shule ya msingi ya  Waasya iliyoko Mwingi ya kati ilifungwa baada ya mwalimu huyo kugunduliwa kuwa na virusi vya Corona mapema wiki hii.

Haya yamejiri majuma machache baada ya shule ya msingi ya Kithumula Kitui magharibi kufungwa baada ya walimu wawili na mwanafunzi kuthibitishwa kuwa na ugonjwa huo.

Hatua ya kufungwa kwa shule hiyo ilithibitishwa na mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Kitui Salesa Adano.

Adano aliwahakikishia wazazi kwamba wanafunzi wote walipimwa na maafisa wa afya ya umma.

Kwa kujibu wa mkurugenzi huyo, shughuli za masomo zitarejelewa kufikia siku ya Jumatatu baada ya matokeo ya waliopimwa kuthibitishwa.

Mkurugenzi huyo wa elimu alisema mwalimu huyo alikuwa miongoni mwa walimu wengine kumi ambao pia baada ya kupimwa waligunduliwa kuambukizwa virusi hivyo vya Covid-19.

Categories
Habari

Sehemu za ibada zatahadharishwa dhidi ya kukiuka sheria za kudhibiti Covid-19

Baraza la dini mbali mbali kaunti ya Embu limeonya makanisa yanayokiuka kanuni za afya kuhusu ugonjwa wa Covid-19 kwamba yatafungwa.

Hata hivyo, akiongea na wanahabari wakati wa mkutano katika kaunti ya Embu Ijumaa, askofu Paul Kariuki wa dayosisi ya kanisa katoliki ya Embu, aliye pia katibu wa baraza hilo, alisema sehemu nyingi za kuabudu zinazingatia kanuni hizo.

Aidha askofu Kariuki alisema katika maeneo ya kijamii kama vile masoko na vituo vya basi, kuna ulegevu katika uzingatiaji kanuni hizo za afya.  

Kiongozi huyo wa dini alitoa wito kwa raia wahakikishe kwamba wanazingatia maongozi hayo huku taifa hili likikumbwa na msururu wa pili wa ugonjwa wa covid-19.

Askofu Kariuki pia aliwahimiza wakazi kwenda katika vituo vya afya wanapohisi dalili za ugonjwa wa covid-19.

Alisema baraza hilo linashirikiana na idara ya afya ya kaunti hiyo ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.   

Categories
Kimataifa

Watu 337 wahukumiwa vifungo vya maisha gerezani nchini Uturuki

Mahakama moja nchini uturuki imewahukumu vifungo vya maisha gerezani maafisa 337 wa kijeshi pamoja na watu wengine katika mojawapo wa kesi kubwa zaidi zinazohusiana na jaribio la mapinduzi ya serikali mwaka 2016.

Marubani wa ndege za vikosi vya angani na makamanda wa kijeshi ni miongoni mwa takriban washtakiwa 500 walioshtakiwa kwa kujaribu kupindua serikali ya rais  Recep Tayyip Erdogan.

Yadaiwa kwamba waliongoza njama hiyo kutoka kwenye kituo cha jeshi la angani cha  Akinci viungani mwa jiji kuu Ankara.

Erdogan alisema kuwa mhubiri mmoja wa kiislamu aliye nchini marekani kwa jina Fethullah Gulen alipanga njama hiyo iliyowafanya watu wengi kukamatwa.

Gulen amekanusha kuhusika kwenye jaribio hilo la kupindua serikali lililotekelezwa mwezi Julai mwaka 2016 lililosababisha vifo vya watu 251 huku wengine zaidi ya elfu-2 wakijeruhiwa.

Kesi hiyo ilianza mwezi Agosti mwaka 2017 ambapo mashtaka ni pamoja na kutaka kumuua rais Erdogan na kuteka taasisi kuu za kiserikali.

Categories
Habari

Sonko mashakani huku hoja ya kumbandua ikiwasilishwa katika bunge la kaunti ya Nairobi

Masaibu ya gavana wa Nairobi  Mike Sonko ya kutaka kumwondoa mamlakani yalikithiri huku wanachama wa bunge la kaunti ya Nairobi wakianzisha rasmi mchakato wa kutaka kumfurusha.

Mwakilishi wadi ya Embakasi Michael Ogada aliyewasilisha ilani ya hoja ya kutaka kumwondoa Sonko mamlakani, alisema kuwa wawakilishi 86 wa wadi wametia sahihi zao kunga kono hoja hiyo.

Mpango huo wa kutaka kumwondoa mamlakani umejiri baada ya  Sonko kudinda kutia saini bajeti ya kila mwaka ya kaunti hiyo ya shilingi bilioni-37.5.

Hali hiyo ya kuchelewesha kutia saini bajeti hiyo imeathiri shughuli za halmashauri ya utoaji huduma kwa eneo la jiji la Nairobi ambayo hushughulikia majukumu mengi ya serikali ya kaunti hiyo.

Hii ni mara ya pili ambapo gavana huyo anakabiliwa na hoja ya kutaka kumwondoa mamlakani ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwezi Februari mwaka huu.

Hoja ya kwanza iliwasilishwa na mwakilishi wadi ya Makongeni Peter Imwatok, kwa madai ya ukiukaji mkubwa wa katiba na sheria ya mwaka 2012 kuhusu fedha za umma na pia kushindwa kuthibiti na kusimamia madeni ya umma na kulipia huduma na bidhaa ambazo hazikuwa zimelipiwa.

Hoja ya Imwatok pia ilimshtumu Sonko kwa kudhihirisha utenda kazi duni na kushindwa kutoa uongozi.

Hoja hiyo inahitaji kuungwa mkono na takriban thuluthi mbili ya waakilishi wote wa wadi ili ipitishwe.

Categories
Habari

Wajane wa Murunga waitaka mahakama iwaruhusu wamzike mume wao

Wajane wawili wa marehemu mbunge wa Matungu Justus Murunga wameiomba mahakama iwaruhusu wamzike marehemu mume wao huku wakisubiri uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na mwanamke mmoja anayedai kuwa mkewe.

Christabel na Grace Murunga sasa wanaitaka mahakama itupilie mbali rufaa hiyo ya Agnes Wangui ambayo ilisababisha kusitishwa kwa mazishi hayo kwa muda.

Wangui alisitisha mipango ya mazishi kusubiri matokeo ya uchunguzi wa msimbo jeni au DNA kubaini iwapo watoto wake wawili ni wa marehemu mbunge huyo.

Wajane hao wawili kupitia kwa wakili wao Patrick Lutta walisema kuendelea kuahirishwa kwa mazishi ya mume wao kunazua taharuki isiyofaa kwani uzazi wa watoto hao unaweza kubainishwa kupitia uchunguzi wa DNA.

Wangui anadai kwamba yeye na marehemu mbunge huyo walikuwa na uhusiano na walikuwa na mipango ya kurasimisha ndoa yao.

Mazishi ya marehemu Murunga yalikuwa yafanyike tarehe 28 mwezi huu wa Novemba lakini yakasitishwa na agizo la mahakama baada ya mwanamke mmoja kudai kuwa ana watoto wawili na marehemu mbunge huyo.

Categories
Habari

Watu 10 wafariki kutokana na Covid-19 huku visa 780 vipya vikinakiliwa hapa nchini

Watu 780 wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi cha saa 24 zilizopita kutokana na sampuli 6,158 zilizopimwa.

Idadi hiyo mpya inafikisha idadi jumla ya visa vya Covid-19 hapa nchini kuwa 80,102.

Kwa ujumla taifa hili limepima sampuli 861,561 tangu mwezi Machi mwaka huu wakati kisa cha kwanza kiliripotiwa.

Kati ya visa hivyo vipya, 754 ni wakenya na 26 ni raia wa kigeni ambapo 460 ni wanaume na 320 ni wanawake.

Aliye na umri mdogo zaidi ni mtoto wa mwaka mmoja na mkubwa zaidi ana umri wa miaka 94.

Watu 10 wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo na kufikisha 1,427 jumla ya watu ambao wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Habari njema ni kwamba watu 552 walipona ugonjwa huo ambapo 468 walikuwa kwenye mpango wa kuwahudumia wagonjwa hao nyumbani na 84 waliondoka kutoka hospitali mbali mbali.

Watu 53,526 wamepona ugonjwa huo kufikia sasa hapa nchini.

Kaunti ya Nairobi ingali inaongoza kwa maambukizi ya visa vipya huku ikinakili visa 273, Kiambu 93, Mombasa 86, Busia 85, Nakuru 40, Turkana 32, Uasin Gishu 20, Kilifi 16, Meru, Kajiado na Kericho visa 13 kila moja na Kisumu visa 11.

Categories
Habari

Idadi ya wasichana watakaofanya KCSE mwaka huu kaunti ya Kilifi yapiku ile ya wavulana

Kwa mara ya kwanza Kaunti ya Kilifi imesajili idadi kubwa ya wasichana kuliko wavulana katika mtihani wa KCSE mwaka huu, hatua ambayo imepongezwa na viongozi wa eneo hilo pamoja na maafisa wa elimu.

Kulingana na mkurugenzi wa elimu kaunti ya Kilifi Eunice Khaemba wasichana 19,878 wamesajiliwa kufanya mtihani wa KCSE mwaka huu dhidi ya wavulana 19,508 waliosajiliwa, hii ikiwa kinyume na hapo awali ambapo idadi ya wavulana ilipiku ile ya wasichana.

“Tunashuhudia mabadiliko ya usawa wa kijinsia katika sekta ya elimu licha ya kuwa wasichana wengi wameacha shule kutokana na changamoto ambazo zinashughulikiwa na serikali. Hatua ya kuwasaidia wasichana werevu kutoka familia masikini pia imewapa motisha wasichana hawa,” alisema Khaemba.

Licha ya kuwa kaunti ndogo ya Malindi iliongoza kwa kusajili wasichana 4,332, Khaemba alisema usajili wa wasichana katika kaunti ndogo za Ganze,Magarini na Kaloleni pia umeimarika ambapo zaidi ya wasichana 8,000 wamesajiliwa kwa mtihani huo wa kitaifa.

“Kwa usaidizi wa mashirika yasio ya kiserikali, afisi yangu imeweza kuwafikia baadhi ya wasichana pamoja na wazazi wao na kuwaeleza umuhimu wa elimu. Visa vya wasichana kuacha shule pia vimepungua katika siku za hivi karibuni,” aliongeza Khaemba.

Mwakilishi wanawake kaunti ya Kilifi Getrude Mbeyu alipongeza ongezeko hilo la wasichana kukumbatia elimu huku akiahidi kuwasaidia katika maendeleo yao ya siku za usoni.

Mbeyu aliahidi kuwapa watahiniwa wote wa kike visodo hadi watakapokamilisha mtihani wa KCSE mwezi Aprili mwaka 2021.

“Nawasihi watawala wote kuwatia nguvuni wanaosababisha wasichana kuacha shule kupitia dhuluma za kimapenzi au ndoa za mapema,” alisema Mbeyu.

Categories
Habari

Rais Kenyatta ahimiza vikosi vya KDF kuwa tayari kukabiliana na vitisho vya kiusalama

Rais Uhuru Kenyatta amehimiza vikosi vya ulinzi vya Kenya KDF kuwekeza Zaidi katika mafunzo ili kuboresha ukabilianaji na vitisho vya kiusalama.

Rais aliyasema hayo Alhamisi katika chuo cha mafunzo ya kijeshi cha Lanet kaunti ya Nakuru wakati wa gwaridi ya kufuzu.

“Vikosi vyetu vya ulinzi vinapaswa kuwa tayari kukabiliana na changamoto za aina mbali mbali, kudhibiti kikamilifu changamoto za kiusalama za karne ya 21 na mafunzo ya kijeshi yawiainishwe na changamoto zinanochipuza,” alisema rais.

Kiongozi wa taifa aliwahimiza maafisa hao waliofuzu kuzingatia kiapo chao cha kulinda taifa hili kutokana na aina yoyote ya uvamizi.

Rais alitoa wito kwa maafisa waliofuzu kuzingatia kikamiifu mafunzo waliopokea na  kukumbuka kila mara wajibu wao wa kutumikia taifa hili kwa nidhamu ya hali ya juu.

Chuo cha mafunzo ya kijeshi kimekuwa kikitoa mafunzo kwa maafisa wa cadet katika kanda ya Afrika Mashariki na pia katika mataifa mengine barani Afrika kama vile Botswana, Burundi, Malawi na Swaziland kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa mataifa ya Afrika mashariki.

“Nina hakika kwamba maafisa waliofuzu kutoka mataifa ya Rwanda, Tanzania na Uganda, watarejea katika nchi zao wakiwa na mafunzo ya hali ya juu kutoka kwa tasisi iliyobobea kwa utoaji mafunzo ya kijeshi barani Afrika,” alisema rais.

Rais aliwatuza maafisa waliofanya vyema katika nyanja mbalimbali wakiongozwa na Brian Mathinji Ngure aliyekuwa bora katika uogozi akifuatiwa na Diamu Dida aliyekuwa wa pili.

Gwaride hiyo ya kufuzu pia ilihudhuriwa na gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui, waziri wa ulinzi Monica Juma na mkuu wa vikosi vya KDF Jenerali Robert Kibochi.

Wengine ni pamoja na inspekta jenerali wa polisi Hilary Mutyambai na kamanda wa chuo cha mafunzo ya kijeshi Meja jenerali  Peter Njiru miongoni mwa wengine.

 

 

 

Categories
Kimataifa

Joe Biden ahimiza utulivu msimu wa baridi unapoghubika Marekani

Rais mteule wa Marekani Joe Biden ametoa wito wa kudumishwa kwa amani  nchini humo hasa wakati huu wa msimu wa baridi unaondamana na msambao wa  virusi vya  Corona.

Kwenye hotuba ya kuadhimisha likizo ya kutoa shukrani,Biden alisema  sasa ni wakati wa kupambana na virusi vya Corona na siyo kugawanyika.

Aliwahimiza raia wa nchi hiyo kuzingatia maagizo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.

Hayo yanajiri huku Rais Donald Trump akiwahimiza wafuasi wake kufanya kila juhudi kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais nchini humo.

Akiongea kwa njia ya simu kutoka ikulu ya White House wakati wa hafla ya wabunge wa chama cha Republican huko  Pennsylvania, Trump alirejelea madai yake kwamba uchaguzi huo ulikuwa na dosari tele.

Trump alikuwa ametarajiwa kuhudhuria hafla hiyo lakini akaahirisha safari hiyo baada ya wandani wawili wa wakili wake Rudy Giuliani kuambukizwa virusi vya Corona, lakini Giuliani alihudhuria hafla hiyo.

Juhudi za Rais Trump za kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo zimegonga mwamba katika baadhi ya majimbo ya nchi hiyo.