Categories
Burudani

Nisamehe!

Mwanamuziki wa Tanzania Harmorapa ameomba msamaha kwa mwanamuziki mwenza Amber Lulu, mtoto wake, baba ya mtoto huyo na umma.

Hii ni baada yake kutangaza kwenye mitandao ya kijamii kwamba yeye ndiye baba mzazi wa mtoto wa Amber jambo ambalo sio la kweli.

Amber alikasirishwa na kitendo cha Harmorapa na alipohojiwa na wanahabari alibubujikwa na machozi akisema atamchukulia hatua za kisheria Harmorapa.

Mambo yalianza baada ya Amber kutambulisha mtoto wake kwa mara ya kwanza kwa umma kupitia picha walizopigwa kwa ajili ya kuwa mabalozi wa bidhaa za watoto.

Siku ya kutangaza kazi hiyo Amber alialika wanahabari ambapo alisema kama utani tu kwamba ana wasiwasi kuhusu baba mtoto.

Harmorapa akaona amepata mwanya wa kutafuta umaarufu mitandaoni kupitia Amber na mtoto wake.

Kufikia sasa Harmorapa amefuta picha zote ambazo alikuwa amepachika kwenye akaunti yake ya Instagram kama njia ya kutaka kuaminisha umma kwamba mtoto ni wake.
Kwenye video ya kuomba msamaha, wanahabari wanasikika wakimpa maneno ya kusema huku wakiwa na hasira.

Baadaye alionekana akitangaza wimbo wake kwa jina “Sina adabu” ambao anasihi mashabiki wakautazame kwenye You Tube.

Wawili hao, Amber na Harmorapa waliangaziwa kwenye kipindi cha runginga ya Wasafi ya Tanzania.

Categories
Burudani

ICM yalaumiwa kwa ubaguzi

Shirika la ICM Partners ambalo ni mshirika mkuu wa Hollywood ambayo ni sekta ya filamu nchini Marekani limejipata pabaya baada ya tetesi kuibuka kuhusu ubaguzi uliopo.

Hii ni baada ya wafanyikazi wa sasa na wa zamani wa shirika hilo wapatao 30 kutoa ushuhuda kuhusu mateso dhidi ya wanawake na ubaguzi wa rangi ambao walipitia kwenye shirika hilo.

Kampuni ya ICM Partners ambayo kazi yake ni kuwakilisha wateja mbali mbali kama vile wanaotayarisha filamu, vituo vya runinga, wanamuziki, wachapishaji kati ya wengine wengi katika sekta nzima ya burudani, inasemekana kutojali wafanyikazi wasio wazungu pamoja na wanawake.

Jabari McDonald ambaye aliwahi kufanya kazi kwenye shirika la ICM anasema wafanyikazi weusi au ukipenda wenye asili ya Afrika, hutumiwa tu kuleta dhana kwamba watu wenye rangi hiyo ya ngozi wanashirikishwa lakini hali halisi ni tofauti.

Anasimulia kisa ambapo yeye na wenzake wawili walitumiwa kuunda video ya kuadhimisha mwezi wa historia ya watu weusi mwaka 2019 ili kuonyesha kwamba mpango wa shirika la ICM wa mafunzo kwa maajenti unashirikisha wote.

Hatimaye yeye na wenzake hawakujiona kwenye video ya mwisho iliyotumika, walikatwa.

Mwaka 2019 ndio ICM ilichagua mwanachama wa kwanza mweusi wa bodi kwa jina Lorrie Bartlett na kati ya washirika na wakurugenzi 60, weusi ni wanne tu!

Katika kujitetea, ICM kupitia taarifa imesema kwamba haivumilii mateso, ubaguzi au vitendo vyovyote vya kudhalilisha na kwamba afisi yake ya raslimali watu huchunguza ripoti za visa kama hivyo na kuchukua hatua.

Hatua hizo ICM inadai zinajumuisha kufuta kazi watekelezaji wa matendo mabaya dhidi ya wenzao.

Categories
Burudani

Nyce Wanjeri atoa kibao chake cha kwanza

Muigizaji Nyce Wanjeri maarufu kama “Shiro” ametoa kibao chake cha kwanza kiitwacho “Nakuhitaji” anapoanza safari rasmi kama mwanamuziki.

Nyce amemhusisha mpenzi wake aitwaye Leting kwenye kibao hicho. Leting ni mwimbaji na pia anacheza gitaa katika kundi la watu watatu liitwalo Halisi Nation.

Akitangaza ujio wa wimbo huo ambao aliuachilia leo saa sita mchana kwenye mtandao wa You Tube, Nyce aliutaja kuwa wimbo wa shukrani kwa Mungu kwani amemtoa mbali.

Kando na kibao hicho chake binafsi amehusishwa na wanamuziki Vivian na Prezzo kwenye kibao kiitwacho “Uko tu Sawa” ambacho kiliachiliwa wiki jana kwenye You Tube.

Video ya kibao “Nakuhitaji” inaanza na onyesho la tukio ambapo Nyce alituzwa jijini Lagos nchini Nigeria miaka miwili iliyopita.

Alishinda katika kitengo cha muigizaji bora wa kike kwenye ucheshi na vipindi vya runinga chini ya tuzo za Africa Magic Viewers’ Choice Awards yaani AMVCA.

Kwenye hotuba yake mwaka huo, alifichua kwamba kwa aliabiri ndege kwa mara ya kwanza maishani kuelekea Nigeria na ndilo lilikuwa tuzo lake la kwanza maishani.

Binti ya Nyce kwa jina Natasha Nyawira naye amehusishwa kwenye video hiyo.

Awali, Nyce alikuwa kwenye ndoa na bwana mmoja kwa jina Titus Wagithomo ambaye alijitokeza mwaka 2018 kutangaza kwamba ndoa yao ilikuwa imefikia mwisho huku akimlaumu Nyce kwa kutelekeza majukumu yake kama mke na mama hasa baada ya kupata ufanisi katika kazi yake.

Categories
Burudani

Weezdom aacha kazi kama meneja wa Bahati

Msanii Lawrence Munyao maarufu kama Weezdom amesema kwamba ameacha kazi rasmi kama meneja wa msanii Bahati na kampuni yake ya EMB records.

Akizungumza na watangazaji Bonnie Bonnie na Cynthy Cynthy kwenye kipindi cha Zinga la Asubuhi ndani ya KBC Radio Taifa, Weezdom alielezea kwamba hatua yake ya kujiuzulu inatokana na ari ya kukua katika sekta ya burudani.

Alifichua kwamba ataendeleza kazi yake kama meneja wa wasanii mbali mbali, chini ya kampuni ambayo atazindua karibuni.

Kazi yake ya mwisho chini ya EMB records ni albamu ya kwanza ya Bahati “Bahati The Album” ambayo bado haijazinduliwa rasmi.

Baadhi ya mashabiki walikisia kwamba Weezdom amekosana na Bahati kwa mara nyingine lakini alitupilia mbali madai hayo akisema wanasalia kuwa marafiki.

Anaendelea kushukuru Bahati kwa kugundua talanta yake na kumpa nafasi ya kukua kama mwanamuziki na meneja chini ya EMB Records.

Weezdom na Bahati awali walikuwa wakiimba nyimbo za injili kabla ya kuingilia nyimbo za kidunia.

Wa kwanza kutangaza hatua hiyo ni Weezdom mwezi Aprili mwaka 2020 na kufikia mwezi Julai mwaka huo, Bahati naye anatangaza kuacha kuimba nyimbo za injili.

Weezdom hajatoa kibao tangu kuachana na nyimbo za injili lakini Bahati ana nyingi ambazo zinaangazia mapenzi.

Wawili hao wanahisi kwamba Kuna uozo mwingi katika sekta ya muziki wa injili.

Categories
Burudani

Visita anaomba usaidizi!

Mwanamuziki Visita ambaye pia ni mtayarishaji wa muziki anaomba usaidizi kutoka kwa wakenya. Hii ni baada yake kushindwa kulipa kodi ya nyumba na kukosa ada za hospitali.

Chanzo cha masaibu yake kulingana naye, ni ujio wa janga la Corona ambalo lilisababisha maeneo ya burudani kufungwa na hiyo ndiyo sehemu alikuwa akijipatia riziki.

Visita ambaye jina lake halisi ni Nixon Wesonga anajulikana kwa kutayarisha vibao vingi kama vile Fimbo Chapa kibao cha wanamuziki wa kampuni ya Grandpa Records na Kamua leo ambao awali ulikuwa wa Kidis peke yake na akaurudia kwa ushirikiano na wanamuziki wa kampuni hiyo ya Grandpa.

Alisema wasanii wengi wanapitia magumu kimya kimya lakini yeye ameamua kupaaza sauti na kuomba usaidizi kwani ana mke na watoto wawili ambao anafaa kulisha na hajalipa kodi ya nyumba kwa muda mrefu.

Mwanamuziki huyo ambaye anaishi katika eneo la Roysambu alielezea pia kwamba hajihisi vizuri lakini alipokwenda hospitali alihitajika kulipia huduma kabla na hakuwa na pesa zozote.

Juzi msanii mwingine kwa jina Justina Syokau maarufu kwa nyimbo zake za kukaribisha mwaka mpya za Twendi Twendi na Twendi Tweni One alijitokeza kuomba usaidizi akisema ameugua kwa muda na anahitaji usaidizi kulipa ada ya hospitali ambayo imefikia milioni mbili.

Categories
Burudani

Meghan Markle aandika kitabu cha watoto

Meghan Markle ambaye alikuwa muigizaji kabla ya kukutana na mwanamfalme wa Uingereza Harry na baadaye kuolewa naye, ameandika kitabu cha watoto. Kitabu hicho kinaangazia uhusiano kati ya baba na mwanawe jinsi auonavyo mama ya mtoto huyo.

Kitabu hicho kwa jina “The Bench” kimetokana na maisha ya familia yake changa, yeye, mume wake Harru na mwanao Archie.

Kupitia taarifa, Meghan alielezea kwamba kwanza alianza kwa kumwandikia mume wake shairi siku ya kina baba ulimwenguni na shairi hilo sasa limegeuka kuwa kitabu.

Meghan ameshirikiana na Christian Robinson mchoraji wa picha hasa za vitabu vya watoto katika kuonyesha uhusiano mzuri kati ya baba na wanawe kwenye kitabu hicho.

Mke huyo wa mwanamfalme anatumai kwamba kitabu cha “The Bench” kitagusa kila familia kwa njia nzuri.

Kampuni ya uchapishaji kwa jina Penguin Random House iliyoko Marekani, kupitia taarifa ilisifia kitabu hicho ikisema kinaangazia uhusiano unaobadilika wa kina baba na watoto wao wa kiume jambo ambalo linakumbusha wengi kuhusu njia tofauti upendo unaweza kudhihirika katika familia ya kisasa.

Meghan atatia sauti kitabu hicho ambacho kitazinduliwa rasmi tarehe 8 mwezi Juni mwaka huu ili kufikia wale ambao hawapendi kusoma lakini wanaweza kusikiliza.

Meghan na mume wake Harry waliamua kujitenga na familia ya Ufalme na hivyo kuacha majukumu yote ya familia hiyo. Uamuzi wao utasababisha ufadhili kutoka kwa familia ya ufalme kukomeshwa kabisa na hivyo basi wawili hao lazima watafute njia ya kujikimu kimaisha.

Walipohamia Canada kisha Marekani, duru ziliarifu kwamba walikuwa wakitumia pesa ambazo Harry aliachiwa na mamake mzazi marehemu “Princess Diana”.

Categories
Burudani

“Sikuiga Michael Jackson” asema Jay Styles

Mwanamitindo ya mavazi nchini Tanzania Jay Styles ameangaziwa sana kwa siku chache zilizopita kutokana na kazi yake ya vazi ambalo Harmonize alivaa kwenye video ya wimbo wake wa “Attitude”.

Kwenye video ya wimbo huo ambao amemhusisha Awilo Longomba na H Baba, Harmonize anaonekana akiwa amevaa koti ambayo imetiwa vijiko, umma na visu kama mapambo.

Watafiti wa mitandaoni hata hivyo waligundua kwamba wazo la ubunifu huo sio jipya kwani mwanamuziki Michael Jackson ambaye aliaga dunia mwaka 2009 alikuwa na vazi sawia.

Koti hiyo ya Michael Jackson ilipatiwa jina la “Dinner Jacket” na iliundwa na mwanamitindo Michael Lee Bush. Mwaka 2018 koti hiyo ya marehemu Michael Jackson ilikuwa mojawapo ya vitu vilivyoonyeshwa kwenye maonyesho kwa heshima yake mjini London nchini Uingereza.

Jay Styles ambaye ni mwanamitindo rasmi wa Harmonize na kundi lake la Konde Gang amejitetea akisema hakuigiza vazi la Michael Jackson lakini anafurahia kwamba vazi lake limeenea.

Ikumbukwe kwamba Michael Jackson alimiliki vazi hilo miaka mingi iliyopita.

Watu wengi wamekuwa wakitania vazi hilo la Harmonize kama vile wachekeshaji wa Kenya Eric Omondi na Eunice Mamito. Wawili hao walichukua hatua ya kuongeza vyombo vingine vya jikoni kwenye mavazi yao.

Akihojiwa na kituo kimoja cha redio nchini Tanzania, Jay Styles alisema kwamba aliunda vazi hilo kitambo lakini Harmonize akamwambia waliweke watalitumia kwa kazi kubwa siku za usoni.

Categories
Burudani

Otile Brown afurahia ufanisi wa nyimbo zake kwenye You Tube

Mwanamuziki Jacob Obunga maarufu kama Otile Brown ni mwingi wa furaha baada ya nyimbo zake mbili kuchukua nafasi ya kwanza na ya pili kwenye orodha ya nyimbo za Kenya zilizotizamwa sana kwenye mtandao wa You Tube.

Kwenye akaunti yake ya Instagram, Otile alichapisha picha za video za nyimbo hizo mbili jinsi zilivyo kwenye You Tube. Picha ya kwanza ni ya wimbo “Dusuma” ambao amemhusisha Meddy na ambao umetizamwa mara milioni 26.

Ya pili ni ya wimbo “Chaguo la moyo” ambao amemhusisha Sanaipei Tande ambao umetizamwa mara milioni 25 kwenye mtandao huo wa You Tube.

Otile alishukuru wanamuziki wensa Meddy na Sanaipei na mashabiki wake wote. Alisema huwa wanatambua na kuthamini usaidizi wao.

Video ya Dusuma imetizamwa mara milioni 6 tangia Januari tarehe 17. Siku hiyo ilikuwa imetizamwa mara milioni 20 na sasa imetizamwa mara milioni 26.

Wakati mwanamuziki Octopizzo alionekana kutoridhishwa na hatua ya wakenya kupendelea wanamuziki wa Tanzania kama Diamond Platnumz, Otile kwa upande wake aliunga mkono wakenya akiwasihi wampende watakaye.

Wakati huo alidai kwamba wivu ni ishara ya udhaifu na kuhimiza wanamuziki wafanye kazi nzuri ambayo itapendeka na wengi.

Alitoa wito kwa watangazaji pia kuupa muziki mzuri nafasi hata kama ni wa mwanamuziki anayeibukia.

Categories
Burudani

Will Smith aingia kwenye mkataba na You Tube anapoanza safari ya kupunguza uzani wa mwili

Muigizaji wa Marekani Will Smith alichapisha picha yake kwenye akaunti yake ya Instagram akielezea kwamba aliongeza uzani wa mwili kutokana na jinsi alikuwa akila wakati wa kujitenga kwa sababu ya virusi vya Corona.

Alisema anapenda mwili wake lakini angependa kuwa bora huku akikatiza hulka ya kula hata usiku wa manane. Hapo ndipo alifichua kwamba safari yake ya kupata mwili ulio bora na kupata afya njema itakuwa kwa ushirikiano na mtandao wa You Tube.

Mwaka 2019, Will Smith alizungumzia uzani wa mwili wake ambao alisema ulikuwa umezidi kiwango cha kawaida na akaonyesha nia ya kuanzisha mpango wa kuupunguza.

Alikuwa akihojiwa na mke wake Jada Pinkett Smith wakati huo kwenye kipindi chake cha Ted Table Talk ambapo alifichia kwamba alikuwa akila keki tano ndogo kwa kiamsha kinywa, chamcha anakunywa mchanganyiko wa pombe mtindo alioendeleza kwa siku kumi mfululizo.

Wakati huo uzani wake ulifikia paundi 225 sawa na kilo 102.

Smith wa umri wa miaka 52, ambaye amewahi kutajwa kuwa mmoja wa wanaume wazuri mno duniani alisema kwamba ongezeko la uzani wa mwili lilitokana na likizo.

Alifunguka na kukiri kwamba kwa miaka 50 ya kuwepo duniani hakujua kwamba mtu ni anachokula yaani mwili utaonyesha jinsi mtu anakula. Alisema alitegemea chakula jinsi wengine hutegemea madawa ya kulevya .

Alikula kupitisha muda na wakati wa furaha pia.

Categories
Burudani

Wasanii Tanzania wapinga kanuni mpya za BASATA

Wasanii wa muziki nchini Tanzania wanaonekana kughadhabishwa na Kanuni na sheria mpya za BASATA kuhusu taratibu za kuandaa na kutoa muziki kwa umma.

Baraza hilo la Sanaa la Tanzania liliamua kwamba kila mwanamuziki ni lazima apeleke wimbo wake kwa afisi zao ukaguliwe kabla ya kuachiliwa kwa umma.

Hatua hii inalenga kuhakikisha maadili yanazingatiwa na kwamba muziki mchafu unazuiwa usisambae.

Mbunge wa Tanga Hamis Mohammed Mwinjuma maarufu kama Mwana Fa ambaye pia ni mwanamuziki amepinga kanuni mpya za BASATA akisema hazina tija na hazisaidii msanii yeyote.

Kwa maoni yake sheria hizo hazistahili kuwepo na kutumika. Analitaka baraza hilo kutafuta namna nyingine ya kuzuia nyimbo chafu na za matusi akifichua kwamba swala hilo liliwahi kujitokeza wakati akihudumu kwenye bodi ya BASATA akalipinga na ataendelea kulipinga.

Anahimiza BASATA kutekeleza sheria nambari 7 ya mwaka 1999 ambayo inatoa idhini kwa shirika linaloshughulikia hakimiliki za wanamuziki COSOTA kutoa leseni kwa maeneo ambayo hutumia muziki na kukusanya hela hizo na kuzitoa kwa wasanii.

“Msifanye kutoa wimbo iwe kama kuomba passport au VISA, mnaonea wasanii,tunakwamisha sanaa.” ndiyo baadhi ya maneno aliyoandika Mwana Fa kwenye Instagram.

Mwanamuziki AY alimuunga mkono Mwana Fa akitaka kujua ikiwa BASATA itazuia nyimbo chafu za Tanzania na kuruhusu za nje kuendelea kuchezwa.

Haya yanajiri wakati msanii wa kwanza ameshajipata pabaya kutokana na kanuni hizo mpya za BASATA.

Msanii Nay wa Mitego alipeleka wimbo wake mpya kwa jina “Mama” kukaguliwa BASATA kabla ya kuutoa kwa umma ukazuiwa. Kisa na maana ni baadhi ya maneno aliyotumia kwenye wimbo kama vile “Shangazi Halima” na “Baba alikuwa mkali”.