Categories
Kimataifa

Armenia yaishtumu Uturuki kwa kukomesha ndege za misaada ya dharura kutumia anga yake

Armenia leo imeishtumu Uturuki kwa kuzuia ndege zinazosafirisha misaada ya dharura kutumia anga yake.

Azerbaijan na Armenia zimeshtumiana kwa kukiuka mkataba wa kukomesha vita uliopatanishwa chini ya juma moja lililopita ili kuwezesha pande hizo mbili kubadilishana wafungwa na miili ya wale waliouawa kwenye makabiliano yaliyozuka tarehe 27 mwezi uliopita.

Makabiliano hayo ndio mabaya zaidi tangu miaka ya tisni ambapo watu elfu-30 waliuwa kwenye vita kuhusiana na eneo la Nagorno-Karabakh ambalo hutambulika kimataifa kuwa sehemu ya Azerbaijan lakini linalotawaliwa na waarmenia.

Wizara ya Azerbaijan imesema kuwa jeshi lake linaendeleza shughuli zake kwenye mpaka wa Nagorno-Karabakh, lakini ikasema taharuki inazidi kutanda kwenye maeneo ya Aghdere-Aghdam na Fizuli-Hadrut-Jabrail.

Wizara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni ya Uturuki ambayo hushughulikia maswala kuhusu anga haikutoa kauli mara moja kuhusu shutma hizo.

Categories
Habari

KBC Channel 1 pekee kupeperusha sherehe ya kufuzu ya KDF

Rais Uhuru Kenyatta ataongoza sherehe ya kufuzu kwa Vikosi vya Kijeshi vya Kenya (KDF) Alhamisi tarehe 24 Septemba, 2020 katika kambi ya wanajeshi ya Moi Barracks huko Eldoret.


Runinga ya KBC Channel 1 ndiyo stesheni pekee itakayopeperusha mubashara au ukipenda moja kwa moja sherehe hiyo inafanyika wakati Kenya na ulimwengu kwa ujumla ikiendelea kushuhudia kuongezeka kwa maambukizi mapya ya virusi vya Covid-19.

Ingawa KDF itatekeleza kikamilifu sheria za Wizara ya Afya za kuzuia msambao wa Covid-19, wananchi hawataruhusiwa kuingia kwenye kambi ya Moi Barracks ya Kikosi cha Tisa (9th Battalion) kushuhudia sherehe hizo kama ilivyo ada huku familia za mahafali zikitakiwa kufuatilia kupitia Runinga ya KBC Channel 1.

*Imeandikwa na Tom Mathinji.

 

 

Categories
Habari

Watu wanne wakamatwa kwa kuhusika kwa wizi wa magari Mombasa na Nairobi

Watu wanne wanaoshtumiwa kwa kuiba magari katika miji ya Mombasa na Nairobi wamekamatwa.

Watatu kati yao ni sehemu ya genge ambalo limekuwa likijisingizia kuwa wateja wanaotaka kukodi magari na baadaye kuyaiba. Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi George Kinoti amesema kuwa gari lililoibwa miezi miwili iliyopita lilipatikana kutoka kwa washukiwa hao.

Washukiwa hao walikuwa wamevuruga mtambo wa kufuatilia gari hilo.

Categories
Habari Uncategorised

Familia 2000 zajisajili kwa bima NHIF

Familia elfu mbili katika eneo-bunge la Mandera Mashariki katika Kaunti ya Mandera zimejumuishwa kwenye mradi wa hazina ya kitaifa ya bima ya matibabu-NHIF.

Akiongea baada ya kukabidhi hundi ya thamani ya shilingi milioni 12 kwa tawi la Mandera la NHIF, Mbunge wa eneo hilo Omar Salah alisema hatua hiyo inanuiwa kupunguza mzigo wa gharama ya matibabu kwa familia nyingi katika eneo bunge hilo.

Alisema hiyo ni njia moja ya kuafikia mpango wa upatikanaji wa matibabu bora kwa wote kuambatana na ajenda nne kuu za serikali. Salah alihimiza hospitali ambako watakaonufaika watatafuta huduma kutoongeza gharama za matibabu.

Meneja wa hazina ya NHIF katika eneo hilo Ahmed Yaqub alisema kadi za watakaunufaika zitakuwa tayari kaunzia wiki ijayo. Wakazi wengi kutoka familia maskini ambao hawangeweza kumudu gharama ya matibabu walikuwa wakitegemea matibabu ya kiasili ambayo wakati mwingi hayakufaulu.

Categories
Vipindi

Marwa amesisitiza fedha billion 8.5 zilizotolewa na serikali kwa wazee na walemavu zitawifikia

Katibu wa Huduma za Jamii Nelson Marwa amesisitiza fedha billion 8.5 zilizotolewa na serikali kwa wazee na walemavu zitawifikia hivi karibuni.

Akizungumza na Wanahabari wa Radio Taifa Bernard Maranga na Cynthia Anyango, Marwa aliongeza kuwa wizara ya Leba itakabiliana na wale wanaotumia walemavu au watoto kujinufaisha.

https://podcasts.kbc.co.ke/wp-content/uploads/2020/04/PS-SOCIAL-PROTECTION-NELSON-MARWA-RADIO-TAIFA-23RD-APRIL-2020.mp3
Categories
Habari

Polisi wakomesha mkutano wa kisiasa Kitui

Polisi huko Kitui walirusha vitoza machozi na kutawanya mikutano ya kisiasa iliyokuwa imeandaliwa na wabunge wa Ukambani wanaoegemea upande wa Naibu wa Rais Wiliam Ruto.

Matatizo yalianza wakati wabunge hao wakiongozwa na mbunge wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai, waliposimama katika soko la Mathima lililoko Kitui Kusini ambako walitaka kupigia debe ajenda ya Naibu wa Rais ya mwaka 2022.

Wabunge wengine walikuwa mbunge wa Machakos mjini Victor Munyaka, Vincent Musyoka wa (Mwala), na Fabian Kyule wa (Kangundo).

Wabunge hao walijaribu kushauriana na maafisa wa polisi bila mafanikio. Walirusha vitoza machozi huku watu wakiendelea kukusanyika katika soko hilo na kuwatawanya hata kabla ya mkutano huo wa hadhara kuanza.

Viongozi hao walilalamikia hatua ya kuwanyima fursa ya kuwahutubia wananchi wakisema hatua hiyo inakiuka uhuru wa kikatiba wa kukusanyika na kutoa maoni.

Mbai alisema ziara yao ya kukutana na watu haikuwa na hila zozote na polisi hawakuwa na haki ya kuwatawanya.

Categories
Habari

Nalaumu wapinzani wangu kwa tuhuma za ufisadi – Ojaamong asema

Gavana wa Kaunti ya Busia Sospeter Ojaamong anasema tuhuma za ufisadi dhidi yake zilichochewa na mahasimu wake wa kisiasa.

Ojaamong aliyekuwa akiongea katika Kijiji cha Kocholya, Kaunti Ndogo ya Teso Kaskazini alisema njama ya wapinzani yake haitafaulu.

Alisema kukosa kwa serikali ya taifa kutoa pesa zinazogawiwa kaunti kunarudisha nyuma maendeleo katika eneo hilo. Alisema serikali ya kaunti ina pesa za kuwalipa wafanyikazi wake mishahara ya mwezi huu pekee na akatahadharisha kwamba ikiwa serikali haitatoa pesa hizo, shughuli za kaunti zitakwama.

Ojaamong alisema atashirikiana na viongozi wa eneo hilo akiwemo mbunge, Oku Kaunya kuimarisha taasisi za afya kama vile zahanati ya Malaba na hospitali ya kaunti ndogo ya Kocholya ili kuimarisha huduma za afya.

Kaunya alisema mipango inaendelea ya kuipandisha hadhi hospitali ya kaunti ndogo ya Kocholya kuwa ya kiwango cha Level Five.

Categories
Michezo

Manchester United iko tayari kusitisha usajili wa Jadon Sancho

Timu ya Manchester United inayoshiriki katika ligi kuu ya soka nchini Uingereza imesema iko tayari kusitisha harakati za kuwania usajili wa winga Jadon Sancho.

Dortmund inataka malipo ya pauni milioni 108 huku United almaarufu ‘ The Red Devils’ ikisisitiza kuwa haiwezi kulipa zaidi ya pauni milioni 80.

Wakati uo huo , mchezaji Kevin-Prince Boateng amepewa kandarasi ya miaka mitatu na timu aliyoichezea awali Las Palmas.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ghana aliichezea Las Palmas kwa mwaka mmoja kabla ya kujiunga na Eintracht Frankfurt, kisha Sassuolo na Fiorentina.

Categories
Habari

Oparanya aonya kaunti zote zitasimamisha huduma Alhamisi iwapo mzozo wa ugavi utakuwepo

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya ameonya kwamba ifikapo Alhamisi wiki ijayo, serikali za kaunti zote 47 nchini zitasimamisha huduma zao iwapo mzozo kuhusu mfumo wa ugavi wa pesa kwa serikali za kaunti hautakuwa umesuluhishwa.

Oparanya ametoa wito kwa Bunge la Seneti lisuluhishe mzozo huo haraka iwezekanavyo.

Alikuwa akiongea katika makao makuu ya Kanisa la Church Of God yaliyoko kima katika Kaunti ya Vihiga wakati wa ibada ya mazishi ya Askofu Dkt. Byrum Makokha.

Matamshi yake yaliungwa mkono na kiongozi wa Chama cha ANC Musalia Mudavadi aliyesema iwapo mzozo wa ugavi wa raslimali kwa kaunti hautasuluhishwa haraka, utarudisha nyuma maendeleo ambayo yamepatikana kupitia kwa ugatuzi.

Kuhusu ufisadi, Musalia alimtaka Rais Uhuru Kenyatta ahakikishe wale wote ambao wamehusika na ufisadi wamekamatwa na kushtakiwa ili uchumi wa nchi hii ukue.

Categories
Michezo

Pogba arejea mazoezini

Kiungo wa timu ya Manchester United, Paul Pogba, amerejea mazoezini baada ya kuthibitishwa kuambukizwa virusi vya Korona lakini huenda asicheze katika mechi yao ufunguzi ya ligi kuu ya soka nchini Uingereza dhidi ya Crystal Palace tarehe 19 mwezi huu.

Pogba alitemwa katika kikosi cha Ufaransa kilichoshiriki kwenye michuano ya ligi ya mataifa ya Bara Ulaya dhidi ya Uswidi na Kroatia; baada ya kocha Didier Deschamps, kuthibitisha aliambukizwa virusi vya Korona wakati alipokitaja kikosi chake mwishoni mwa mwezi Agosti.

Aidha, Manchester United imethibitisha kuwa Pogba amepona na tayari amerejea mazoezini. Mchezaji huyo hakucheza kwenye mechi kadhaa msimu uliopita baada ya kujeruhiwa lakini akaichezea United mechi 9 baada ya ligi kuu kurejelewa mwezi Juni, huku akiisaidia timu hiyo kumaliza katika nafasi ya tatu, na kufuzu kwa ligi ya kilabu bingwa Barani Ulaya.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, amehusishwa na kujiunga na Real Madrid au Juventus lakini kwa sasa huenda akasalia uwanjani Old Trafford.