Categories
Kimataifa

Mtandao warejeshwa Uganda baada ya kufungwa wakati wa uchaguzi mkuu

Huduma ya mtandao imerejeshwa nchini Uganda baada ya kuzimwa kwa siku tano wakati wa uchaguzi mkuu.

kufuatia agizo la serikali, huduma hiyo ilifungwa Jumatano usiku, saa chache kabla ya kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura kwenye uchaguzi mkuu wa siku ya Alhamisi iliyopita.

Hata hivyo, mitandao ya kijamii bado imesalia kufungwa.

Wakati uo huo, msemaji wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), Joel Ssenyonyi, amesema afisi ambapo mawakala wake walikuwa wakiandaa stakabadhi za kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo zimevamiwa na wanajeshi.

Ssenyonyi amesema mawakala hao walikuwa wakikusanya fomu za matokeo ya uchaguzi zilizo na ushahidi wa udanganyifu.

Hii ni baada ya makaazi  ya kiongozi wa chama hicho Bobi Wine kuzingirwa na wanajeshi wa serikali.

Bobi alikataa matokeo ya uchaguzi wa urais kama yalivyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo.

Kulingana na matokeo hayo, Rais Yoweri Museveni ndiye aliyeshinda kinyang’anyiro hicho dhidi ya Bobi Wine aliyeibuka wa pili.

Bobi alishtumu vikali jinsi uchaguzi huo ulivyofanywa, huku akidai kwamba ana ushahidi wa kutosha kuhusu visa vya udanganyifu.

Categories
Habari

Mahakama yazuia kuapishwa kwa Anne Kananu kuwa Kaimu Gavana wa Nairobi

Mahakama Kuu imetoa agizo la kuzuia kwa muda, shughuli ya kuapishwa kwa Anne Kananu Mwenda kuwa Kaimu Gavana wa Kaunti ya Nairobi.

Kwa mujibu wa agizo hilo, Kananu hataapishwa hadi kesi iliyowasilishwa na Chama cha Mawakili (LSK) na Tume ya Haki za Kibinadamu humu nchini (KHRC) itakaposikizwa na kuamuliwa.

Aidha, mahakama hiyo imemtaka Kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kuteua jopo la majaji wasiopungua watatu, watakaotoa uamuzi kuhusu kesi hiyo.

Haya yanajiri saa chache tu baada ya Kananu kukabidhiwa wadhifa huo na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura, ambaye alichukua hatamu hizo baada ya kubanduliwa mamlakani kwa aliyekuwa Gavana Mike Sonko.

Mutura alivaa kofia ya Kaimu Gavana kutokana na kutokuwepo kwa naibu gavana katika kaunti hiyo, hatua iliyoashiria kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo kauntini humo.

Hata hivyo, Anne Kananu, aliyeteuliwa na Sonko ili awe naibu wake tangu mwezi Januari mwaka uliopita, alisailiwa na kuidhinishwa Ijumaa iliyopita na Bunge la Kaunti ya Nairobi na hatimaye kuapishwa kuwa Naibu Gavana.

Kulingana na Mutura, kupatikana kwa naibu gavana wa kaunti hiyo kulimaanisha kwamba anafaa kuchukua wadhifa wa kaimu gavana kwa muda uliosalia hadi uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Categories
Habari

Taharuki yatanda Kapedo baada ya afisa wa GSU kuuawa na majambazi

Taharuki imetanda katika eneo la Kapedo kwenye mpaka wa kaunti za Baringo na Turkana, baada ya afisa mmoja wa GSU kuuawa na majambazi.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Baringo Robinson Ndhiwa amethibitisha kisa hicho, akisema afisa huyo alipigwa risasi na majambazi wakati wa uvamizi katika eneo la Ameyen.

Kisa hicho cha hivi punde cha utovu wa usalama chasemekana kimetokea dakika chache baada ya mkutano wa amani na shughuli ya usambazaji chakula iliyotekelezwa na maafisa wa GSU.

Ndhiwa amesema maafisa hao walivamiwa katika eneo la Ameyen, kilomita saba kutoka Kapedo, wakiwa njiani kurejea katika kambi yao.

Wiki moja iliyopita mwanamume mmoja wa umri wa makamo aliuawa na majambazi katika eneo hilo la Kapedo, kufwatia wizi wa mamia ya mifugo kutoka jamii jirani.

Categories
Habari

Maambukizi ya COVID-19 yazidi kushuka huku watu 65 wakipatikana na ugonjwa huo

Kenya imenakili visa vipya 65 vya ugonjwa wa COVID-19 baada ya uchunguzi wa sampuli 2,681 kufanywa katika muda wa masaa 24 yaliyopita.

Jumla ya visa vya maambukizi ya ugonjwa humu nchini imefikia 99,227 kutokana na upimaji wa jumla ya sampuli 1,128,360.

Kulingana na taarifa kutoka Wizara ya Afya, visa vipya 49 ni vya Wakenya ilhali 16 ni vya raia wa kigeni.

Visa 39 ni vya wanaume huku wanawake walioambukizwa wakiwa 26. Mwenye umri mdogo zaidi ni mtoto wa miaka 12 huku mkongwe zaidi akiwa na miaka 92.

Kaunti ya Nairobi imezidi kuongoza kwa visa 53, ikifuatwa na Kajiado kwa visa 3, Mombasa 2, Kitui 2, Uasin Gishu 2, Machakos 1, Kakamega 1 na Murang’a 1.

Wakati uo huo, wagonjwa 77 wamethibitishwa kupona. 60 kati yao walikuwa kwenye mpango wa kuhudumiwa nyumbani huku 17 wakiruhusiwa kuondoka katika vituo mbali mbali vya afya humu nchini.

Jumla ya waliopona sasa imefikia 83,427.

Taarifa hiyo pia imefichua kwamba wagonjwa watatu zaidi wameaga dunia kutokana na COVID-19 na kufikisha idadi ya walioaga dunia humu nchini hadi 1,734.

Kufikia sasa, jumla ya wagonjwa 697 wanahudumiwa hospitalini ambapo 28 kati yao wako kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi, huku wagonjwa wengine 1,680 wakihudumiwa nyumbani.

Categories
Habari

Vyama vya ANC na Ford Kenya kushirikiana kwenye chaguzi ndogo za Kabuchai na Matungu

Chama cha Amani National Congress hakitawasilisha mwaniaji katika uchaguzi mdogo wa Eneo Bunge la Kabuchai.

Chama hicho badala yake kitamuunga mkono mwaniaji wa chama cha Ford Kenya Majimbo Kalasinga, aliyeteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo huo.

Kalasinga tayari ameidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) baada ya kuwasilisha stakabadhi zake kwa tume hiyo mapema Jumatatu.

Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi aliandamana na mwenzake wa chama cha Ford-Kenya Moses Wetangula hadi katika afisi za IEBC kushuhudia Kalasinga akiwasilisha makaratasi ya uteuzi.

Akiongea muda mfupi baada ya kuidhinishwa kwa Kalasinga, Mudavadi alitoa wito kwa wakazi wa eneo la Magharibi kudumisha umoja hasa wakati huu.

Mudavadi na Wetangula baadaye walielekea katika Eneo Bunge la Matungu kushuhudia mwaniaji wa chama cha ANC Pater Nabulindo naye akiwasilisha makaratasi yake ya uteuzi kwa IEBC.

Ford Kenya itamuunga mkono mwaniaji huyo wa ANC katika uchaguzi mdogo wa Matungu.

Categories
Habari

Anne Kananu sasa ndiye Kaimu Gavana wa Nairobi

Siku tatu tu baada ya kuapishwa kuwa Naibu Gavana wa Kaunti ya Nairobi, Anne Kananu Mwenda amepanda ngazi na kuwa Kaimu Gavana wa kaunti hiyo.

Hii ni baada ya Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura kumkabidhi mamlaka hayo aliyoshikilia baada ya Mike Sonko kutimuliwa mamlakani.

Kananu aliandikisha historia kuwa naibu gavana wa kwanza mwanamke katika kaunti hiyo baada ya kuapishwa na Jaji John Mativo siku ya Ijumaa wiki iliyopita.

Aliapishwa baada ya kusailiwa na kuidhinishwa na Bunge la Kaunti hiyo, kufuatia kuondolewa kwa kesi iliyozuia kusailiwa kwake tangu ateuliwe na aliyekuwa Gavana Mike Sonko mnamo Januari mwaka wa 2020.

Kwenye hotuba yake ya kukubali wadhifa huo, Kananu ameahidi kujiepusha na siasa na kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa wakazi wa kaunti ya Nairobi.

Amesema kuwa ataongoza kwa mfano na kushirikiana vyema na Bunge la Kaunti ya Nairobi, serikali ya taifa na uongozi wa shirika la huduma za jiji la Nairobi.

Kananu ametoa wito kwa wakazi wa Nairobi kutoa maoni kuhusu huduma wanazopewa na serikali ya kaunti hiyo.

Haya yanajiri huku baadhi ya viongozi na Wakenya wakitilia shaka uhalali wa mchakato huo, huku Chama cha Mawakili nchini (LSK) kikiapa kuelekea mahakamani kupinga uteuzi wa Kananu kuwa Naibu Gavana wa Nairobi.

Categories
Habari

Uhuru: Niko tayari kuitumikia nchi tena baada ya kustaafu

Rais Uhuru Kenyatta amesema yuko tayari kuitumikia nchi hii katika wadhifa wowote atakapostaafu urais mwaka wa 2022.

“Sina nia ya kubaki uongozini baada ya kustaafu lakini niko tayari kutumikia nchi katika wadhifa wowote,” amesema Rais.

Kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Coro, Rais Kenyatta ameelezea mchakato uliopelekea kuungana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017.

Akitoa wito kwa jamii ya eneo la Mlima Kenya kuunga mkono mchakato wa BBI, kiongozi wa taifa amesema mpango huo ndio utakaotoa suluhu kwa matatizo ambayo yamekuwa yakijirudia kila baada ya uchaguzi mkuu humu nchini.

“Baada ya kila uchaguzi, hali inabadilika kuwa mashindano ya kikabila. Tunahitaji kubadilisha hali hiyo. Tunahitaji suluhu ambapo kila jamii itajumuishwa,” akasema Rais Kenyatta.

Rais pia amewashtumu baadhi ya wanasiasa wanaopinga ripoti ya BBI, huku akifutilia mbali madai kwamba ripoti hiyo inalenga kuwafungia wanasiasa fulani nje ya kiti cha urais mwaka ujao.

“BBI siyo kwa ajili ya Raila bali ni kwa Wakenya ambao watanufaika. Si silaha ya mwaka 2022 bali ni mbinu ya kuafikia Kenya yenye umoja ambapo hakutakuwa tena na mizozo ya kikabila,” akaongeza.

Aidha, Rais ameonyesha kutoridhishwa na malumbano yanayoendelea kati ya ‘wababe’ na ‘mahasla’, akisema kuwa hali hiyo haisaidii.

Pia ametetea kauli yake ya awali kuhusu mfumo wa urais unaozunguka katika jamii zote nchini, akihoji kwamba mfumo huo utahakikisha kwamba jamii zengine pia zinapata nafasi ya uongozi.

Amesema jamii za Mlima Kenya na Kalenjin ndizo zilizoshikilia kiti cha urais tangu uhuru kupatikana na ni wakati wa kutoa nafasi kwa jamii zengine pia zichukue hatamu.

Categories
Habari

Vijana sasa wanaomba miezi sita zaidi ya Kazi Mtaani

Vijana walionufaika na mpango wa serikali wa Kazi Mtaani katika Kaunti ya Isiolo wametoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta kuongeza muda wa utekelezwaji wa mpango huo ili wazidi kunufaika.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wao Adan Hassan na Katibu Mkuu Noor Juma Osman, vijana hao wamekiri kwamba kupitia mpango huo, vijana wengi wamebadilika kutoka kwenye tabia za ulanguzi wa madawa ya kulevya na uhalifu hadi kuwa watu wanaojukumika kiuchumi.

Wamehoji kwamba iwapo mpango huo wa Kazi Mtaani utafikia tamati, basi baadhi yao huenda wakarejelea tabia zao mbaya za awali.

Mpango huo unaofadhiliwa na serikali ya kitaifa ulipangwa kutekelezwa kwa miezi sita na unatarajiwa kufikia tamati mwishoni mwa mwezi huu wa Januari.

Katika Kaunti ya Isiolo pekee, zaidi ya vijana 3,500 wamenufaika kutokana na mpango huo na wamekuwa wakilipwa shilingi 450 kwa siku.

Vijana hao sasa wanamtaka Rais Kenyatta kuwaongezea miezi sita zaidi ili waendelee kuinuka kiuchumi, kwani baadhi yao tayari wameanzisha biashara ndogo ndogo na pia kujiwekea akiba katika vyama vya ushirika.

Kulingana na Noor, iwapo serikali ya kitaifa itasitisha mpango huo, serikali za kaunti zinafaa kuuendeleza ili kuhakikisha kwamba viwango vya usafi vinasalia juu katika mazingira ya kaunti hizo.

“Kama serikali ya kitaifa haitaongeza muda, tunaomba gavana achukue huu mpango ahakikishe hawa vijana hawatarudi nyumbani, wataendelea kufanya kazi,” akasema Noor.

Kazi Mtaani ni moja kati ya mipango iliyowekwa na serikali ya kunasua makundi ya wananchi kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la COVID-19.

Categories
Kimataifa

Malawi yasitisha shughuli za masomo kufuatia ongezeko la maambukizi ya Corona

Shule zote nchini Malawi zitafungwa kwa angalau siku 15 kuanzia Jumatatu, chini ya kanuni mpya za nchi hiyo za kuzuia msambao wa virusi vya Corona.

Rais Lazarus Chakwera, kupitia hotuba yake ya njia ya televisheni, alitangaza pia kafyu ya nyakati za usiku kuanzia saa tatu saa za taifa hilo.

Aidha, alisema mikusanyiko yote haitaruhusiwa kuwa na zaidi ya watu 50.

Malawi inashuhudia kipindi cha maombolezo ya kitaifa kufuatia vifo vya mawaziri wawili kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Mnamo tarehe 12 mwezi huu, nchi hiyo iliwapoteza Waziri wa Serikali za Wilaya Lingson Belekenyama na mwenzake wa Uchukuzi Muhammad Sidik Mia kupitia ugonjwa wa COVID-19.

Thuluthi moja ya visa vyote vya maambukizi ya COVID-19 vilivyonakiliwa nchini Malawi vimenakiliwa Januari.

Rais Chakwera alisema serikali imetenga kiasi kingine cha dola milioni mbili kuwapatia wahudumu wa afya vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo.

Categories
Habari

Polisi wachunguza kisa cha kasisi aliyepatikana ameaga dunia kitandani mwake Narok

Polisi katika Kaunti Ndogo ya Narok Kusini wanachunguza kisa ambapo kasisi mmoja wa Kanisa Katoliki  alipatikana amefariki chumbani mwake Jumapili, katika sehemu ya Ewaso-Nyiro.

Marehemu Kasisi David Mwangi, ambaye awali alikuwa anasimamia eneo la Ewaso-Nyiro,  alipatikana ameaga dunia akiwa kitandani pake.

Kulingana na ripoti, msaidizi wake alikuwa ameenda kumwangalia baada ya kuchelewa kuamka ili apate kiamsha kinywa lakini akagundua kwamba kasisi huyo ameaga dunia.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Narok John Mutoro, alisema hakukuwa na majereha kwenye mwili wa kasisi huyo.

Hata hivyo, Mutoro alisema kulikuwa na kifaa cha kusaidia mtu kupumua karibu na kitanda chake, kumaanisha huenda alikuwa anaugua ugonjwa fulani.

“Katika uchunguzi wetu, tunadhamiria kuzungumza na daktari wake, ambaye atatoa mwangaza zaidi kuhusu hali ya afya ya kasisi huyo,” akasema Mutoro.

Mwili wa kasisi huyo ulipelekwa kwenye hifadhi ya maiti ya hospitali ya matibabu maalum ya Narok, kusubiri upasuaji.

Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho.