Categories
Habari

Gavana Mutua awataka wanaopinga BBI kukoma kuwapotosha Wakenya

Kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap Dkt. Alfred Mutua ametoa wito kwa wale wanaopinga mswada wa BBI kukoma kuwapotosha Wakenya.

Akiongea wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika eneo la Mwala, Mutua ambaye pia ni gavana wa Kaunti ya Machakos, amesema kuwa katiba haibadilishwi kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi bali inafanyiwa marekebisho ili kuiboresha.

Dkt. Mutua ameongeza kuwa katiba mpya itaongeza pesa zinazotengewa kaunti na kuimarisha maslahi ya Wakenya.

“Mnadanganywa kwamba eti tunabadilisha katiba,  hatubadilishi katiba. Hii ni kuongezea vipengele tu kwa katiba iliyopo,” amesema Mutua.

Ametoa wito kwa kaunti zilizosalia kupitisha mswada huo ili uwasilishwe bungeni na baadaye kwa wananchi ambao watatoa uamuzi wa mwisho kupitia kwa kura ya maamuzi.

Categories
Habari

Wakili Kanjama aitaka mahakama itupilie mbali mchakato wa BBI

Wakili Charles Kanjama amewasilisha kesi mahakamani ya kupinga mchakato wa kuidhinisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka wa 2020.

Kwenye ombi lake, wakili huyo anasema ana sababu za kuamini kuwa utaratibu uliotumiwa kukusanya na kuthibitisha saini za mpango wa maridhiano wa BBI haukutimiza masharti ya kikatiba.

Anaitaka mahakama ifutilie mbali uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwamba ilithibitisha saini zilizokusanywa na kupata kwamba mswada huo uliungwa mkono na zaidi ya wapiga kura milioni moja.

Aidha, Kanyama anataka hatua ya Tume ya (IEBC) ya kutuma mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka wa 2020 wa katika mabunge ya kaunti ibatilishwe.

Wakili huyo anadai kwamba aliiandikia barua IEBC akitaka taarifa iwapo tume hiyo ilithibitisha saini za BBI kwa kulinganisha na saini zilizopo tayari na iwapo orodha ya wapiga kura iko na saini za wapiga kura.

Kanjama amesema IEBC ilimjibu kwamba haikuwa na uwezo huo na kwamba haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kufanya uthibitisho wa saini za wapiga kura.

Kulingana na wakili huyo, hatua ya mabunge ya kaunti kuendelea kujadili na kupitisha mswada huo inaibua wasiwasi kuhusu mchakato mzima na kwamba inafaa kusitishwa mara moja kwa sababu mchakato huo unafanyika kinyume cha katiba.

Categories
Habari

Wauguzi waagizwa kusitisha mgomo wao na kurejea kazini mara moja

Ni afueni kwa Wakenya baada ya chama cha kitaifa cha wauguzi (KNUN) kusitisha mgomo wa wauguzi uliodumu kwa karibu miezi mitatu.

Katibu Mkuu wa chama hicho Seth Panyako ametaja agizo la Jaji Maureen Onyango kuwa sababu ya kusitisha mgomo huo na akawataka wahudumu wa afya kurejea kazini kufikia Alhamisi, saa kumi na moja jioni.

Chama cha matabibu nchini pia kilitoa sababu iyo hiyo kilipositisha mgomo wake siku ya Jumanne.

“Wale wahudumu wa afya wote wakiwemo wauguzi ambao wanashiriki mgomo warudi kazini mara moja. Na pia [Jaji Onyango] akaagiza kwamba zile nidhamu zozote ambazo serikali zilikuwa zimewapa wale ambao wanashiriki mgomo zimesimamishwa,” akasema Panyako.

 Panyako hasa amewaarifu wauguzi katika Kaunti za Taita Taveta, Kisumu, Kisii na Busia kwamba madai yote ya kufutwa kazi na kufurushwa kutoka nyumba zao yalisitishwa na mahakama na hivyo basi wapasa kurejea kazini bila kukosa.

Amewahakikishia wauguzi kwamba chama hicho kitaendelea kushinikiza masuala ya wahudumu wa afya ambayo waliwasilisha kwenye ilani yao ya mgomo kupitia mahakama kwani kamati za mashauriano zimeagizwa kuwasilisha ripoti mahakamani katika muda wa siku 30.

Wauguzi waligoma tarehe 7 mwezi Disemba mwaka wa 2020 wakilalamikia mazingira duni ya kikazi na marupurupu.

Categories
Habari

Wizara ya Afya yatangaza visa vyengine 280 vya COVID-19 na vifo vya wagonjwa wawili

Kenya imenakili kiwango cha maambukizi cha zaidi ya asilimia tano baada ya visa 280 vipya vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 kuthibitishwa kutoka kwa sampuli 4,919 zilizopimwa.

Visa hivyo vipya vimetokana na Wakenya 221 na raia 59 wa nchi za kigeni ambapo 173 ni wanaume na 107 ni wanawake, kati ya umri wa miaka mitatu hadi 89.

Jumla ya visa vilivyothibitishwa humu nchini sasa ni 104,780 na vimetokana na upimaji wa jumla ya sampuli 1,278,200.

Watu 713 wamepona kikamilifu, idadi hiyo ikiwa ndiyo kubwa zaidi ya watu waliopona kunakiliwa katika siku za hivi majuzi.

Wagonjwa 676 wamepona walipokuwa wakitibiwa nyumbani na 37 wakaruhusiwa kuondoka kutoka vituo vya afya. Jumla ya watu waliopona sasa imefikia 86,378.

Idadi ya watu waliofariki imefikia

1,839 baada ya wagonjwa wawili zaidi kufariki kutokana na ugonjwa huo.

Kwa sasa wagonjwa

1,495 wanashughulikiwa nyumbani huku 344 wakiwa wamelazwa hospitalini ambapo 55 wako katika kitengo cha wagonjwa mahututi.

Categories
Habari

Mawaziri wa kaunti nao wanadai kuongezwa mishahara na marupurupu

Maafisa wakuu kwenye serikali za kaunti wamehimiza serikali kuratibu upya mishahara na marupurupu yao ili iwiane na ile ya ma-spika wa mabunge ya kaunti.

Maafisa hao wakuu wamewasilisha waraka kwa Tume ya kuwianisha mishahara ya watumishi wa umma (SRC) kushughulikia swala hilo, wakisema mishahara na marupurupu yao haijaongezwa tangu mwaka 2013.

Maafisa hao walikuwa wamekongamana mjini Naivasha ambapo maafisa wapya wa muda walichaguliwa na kupewa jukumu la kushauriana na SRC kuhusu suala hilo.

Wakitaarifu waandishi wa habari baada ya mkutano huo, mwenyekiti wa kundi hilo Hesmond Onsarigo amesema mfumo wa ugatuzi ulianza kutekelezwa mwaka 2013 na wakati huo walikuwa na hadhi sawa na ma-spika wa mabunge ya kaunti.

Onsarigo amesema tayari wameshauriana na magavana ambao wanaunga mkono ombi lao kwa tume ya SRC.

“Tumezungumza na magavana wetu ambao wametuunga mkono kikamilifu na tutaishurutisha tume ya SRC kuangazia swala letu pia,” akasema Onsarigo, ambaye ni Afisa Mkuu wa Idara ya Kilimo katika Kaunti ya Kisii.

Afisa mwengine, Juma Aguko, kutoka Kaunti ya Homa Bay ameeleza kwamba mipango ya kushairiana na SRC kuhusu swala hilo ilisitishwa mwaka jana kufuatia janga la COVID-19 lililosababisha kufutiliwa mbali kwa mikutani na kufungwa kwa afisi kadhaa za serikali.

Categories
Kimataifa

Uganda yakana madai kwamba viongozi wakuu serikalini wamechanjwa kisiri dhidi ya COVID-19

Waziri wa Afya nchini Uganda Jane Aceng amekanusha taarifa kwamba viongozi wa juu wa serikali wamepata chanjo dhidi ya COVID-19 hata kabla ya taifa hilo kupokea rasmi chanjo hizo.

Kwenye ujumbe wa Twitter, Aceng amesema rais na wandani wake wa karibu hawajapokea chanjo hizo jinsi ilivyodaiwa.

Uganda inatarajiwa kupokea dozi laki moja za chanjo kutoka kampuni ya India, AstraZeneca na nyingine 300,000 kutoka kampuni ya Sinopharm ya Uchina.

Hata hivyo, haijathibitishwa ikiwa chanjo hizo zimewasili katika taifa hilo ambalo kufikia sasa limethibitisha visa 40,221 vya COVID-19.

Kumekuwa na mgogoro katika usambazaji wa chanjo hizo duniani, huku Rais wa Rwanda Paul Kagame akikerwa na unafiki na hujuma kwenye usambazaji wa chanjo hizo hasa kwa mataifa yenye kipato cha chini.

Rais Kagame alisema hayo kwenye ujumbe wake baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus kusema kuwa makubaliano kati ya nchi tajiri na watengenezaji wa chanjo hizo yametatiza ununuzi na usambazaji wa chanjo hizo kupitia mpango wa Covax.

Mpango wa Covax unanuia kuhakikisha usawa katika usambazaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 miongoni mwa mataifa yote duniani.

Mnamo mwezi Disemba, vuguvugu la People’s Vaccine Alliance lilionya kwamba asilimia 70 ya mataifa ya kipato cha chini yataweza kutoa chanjo kwa asilimia kumi pekee ya raia wake.

Lilitoa wito kwa kampuni zinazotengeneza chanjo hizo kutoa habari kuhusu teknolojia inayotumika ili kurahisisha utengenezaji na kuwawezesha watu wengi zaidi kupata chanjo hizo.

Categories
Habari

Kamati ya mswada wa BBI yahimiza Bunge kuiga mfano wa wawakilishi wadi ili kuupitisha

Kamati ya kitaifa ya mpango wa BBI imewapongeza wanachama wa mabunge ya kaunti kote nchini kwa kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020.

Kwenye taarifa, kamati hiyo imesema wawakilishi wadi wametekeleza wajibu wao wa kihistoria kwa kukubaliana na mchakato wa marekebisho hayo ya katiba yatakayowezesha taifa hili kusonga mbele.

“Pia tunawashukuru kwa kuisikiliza sauti ya wananchi wakati wa maamuzi yao kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020,” imesema taarifahiyo.

Kamati hiyo pia imewasifu Wakenya kwa kujitolea kwa wingi na kushiriki katika vikao vya ukusanyaji maoni ya umma kuhusu mswada huo, huku wakipuuzilia mbali habari za uongo zinazoenezwa na wanaopinga mchakato huo.

Wanakamati hao wanasema kupitishwa kwa mswada huo kote nchini ni ishara kwamba wananchi wa Kenya wamezungumza kwa sauti moja.

“Ushindi huu mkubwa unaashiria umaarufu wa BBI na ni ishara ya uungwaji mkono wa mswada wa BBI wakati wa kura ya maamuzi,” wakasema.

Na huku mswada huo ukielekea katika hatua ya mbele, kamati hiyo imewaomba wabunge kuzipa kisogo propaganda zinazoenezwa na kuwaiga wawakilishi wadi kwa kupitisha mswada huo katika Bunge la Kitaifa.

Hayo yanajiri huku mabunge zaidi ya kaunti yakiendelea kujadili mswada huo ambao tayari umetimiza masharti ya kikatiba ya kuungwa mkono na angalau mabunge 24 ya kaunti ili kuingia kwenye awamu nyengine.

Kufikia sasa mabunge 41 yamepitisha mswada huo, huku Bunge la Kaunti ya Migori likisalia la pekee lililokataa mswada huo.

Macho sasa yanaelekezwa kwa kaunti tano zilizosalia, ambazo hazijapigia kura mswada huo zikiwemo Nandi, Elgeyo Marakwet, Uasin Gishu, Mandera na Kilifi.

Sheria inasema mabunge ya kaunti yanafaa kuidhinisha rasimu ya mswada huo katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kuwasilishwa.

Mswada huo sasa utawasilishwa kwa Spika Justin Muturi wa Bunge la Kitaifa na Ken Lusaka wa Seneti ili kupitishwa kabla ya kuwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye atatia saini na kuuwasilisha kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa ajili ya kuandaa kura ya maamuzi.

Categories
Habari

Tabasamu kwa wakazi wa Naisoya, Kaunti ya Narok, baada ya serikali kuwapa hati miliki za ardhi

Wakazi wapatao 600 wa eneo la Naisoya, Kaunti Ndogo ya Narok Kusini wamepokea vyeti vyao vya kumiliki ardhi kutoka kwa serikali.

Kamishna wa Kaunti ya Narok Evans Achoki alisema serikali imejitolea kuhakikisha wakazi hao wana vyeti vya kumiliki ardhi ili kuwawezesha kustawisha vipande vyao vya ardhi na kuwakinga dhidi ya wanyakuzi.

Akihutubia wakazi hao kwenye mkutano wa umma uliofanyika katika Kituo cha Afya cha Naisoya, Achoki alisema mizozo kuhusu umiliki ardhi ndiyo iliyochelewesha ugawanyaji wa ardhi na utoaji vyeti hivyo.

Kamishna huyo, aliyekuwa ameambatana na maafisa wa ardhi, Mwenyekiti wa Baraza la Wazeee wa Maasai Kalena Ole Nchoe na Mwakilishi Wadi wa eneo hilo James Kiok, aliwahimiza wakazi kuheshimu mipaka ya ardhi iliyowekwa ili waishi kwa amani.

Msajili wa ardhi wa Kaunti ya Narok Tom Chepkwesy amesema utoaji wa hati miliki hizo ni afueni kubwa kwa wakazi wa Naisoya ambao wamengoja kwa miaka mingi sana ili kupata stakabadhi hizo muhimu.

Chepkwesy amesema baadhi ya walengwa wa stakabadhi hizo walifariki, hivyo jamaa wao wa karibu wanafaa kutembelea afisi za ardhi ili kubadilisha majina ya umiliki.

Ameongeza kuwa hati miliki hizo zilitolewa bila malipo yoyote na kutoa onyo kwa wakazi hao kuripoti mtu yeyote atakayeitisha pesa kabla kuwakabidhi stakabadhi hizo.

Categories
Habari

Rais Kenyatta azindua hazina ya kufadhili uchumi wa vijana wa MbeleNaBiz

Rais Uhuru Kenyatta amezindua mpango wa kibiashara wa MbeleNaBiz wa kuwatuza wajasiria mali chipukizi na uzinduzi wa mpango makhsusi wa hazina ya vijana wa mwaka 2020-2024.

Akisimamia uzinduzi huo katika Uwanja wa Michezo wa Moi Kasarani Jijini Nairobi, Rais Kenyatta amesema serikali itatenga shilingi bilioni 1.3 za kufadhili uchumi wa vijana wa taifa hili.

Kulingana na Rais, kati ya pesa hizo, shilingi milioni 900 zitatolewa kwa wajasiriamali 250 kama ruzuku.

“Jumla ya shilingi milioni 900 zitapewa

Rais pia ametumia fursa hiyo kuhimiza vijana kuunga mkono mpango wa maridhiano wa BBI ambao tayari umeungwa mkono na mabunge 40 ya kaunti.

Amesema kupitishwa kwa mpango huo kutawawezesha vijana kupata pesa na kuhakikisha rasili mali zaidi zinawasilishwa katika maeneo ya magatuzi ili kufadhili maendeleo.

Categories
Kimataifa

Mohamed Bazoum atangazwa kuwa Rais mpya wa Niger

Tume ya uchaguzi Nchini Niger imemtangaza mgombea wa chama kinachotawala nchini humo, Mohamed Bazoum, mshindi wa marudio ya uchaguzi wa urais.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI), Issaka Souna, alitangaza kuwa Bazoum amepata asilimia 55.75 ya kura zilizopigwa mnamo Februari 21.

Bazoum alimshinda rais wa zamani Mahamane Ousmane ambaye alipata asilimia 44.25 ya kura hizo.

Kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo mnamo tarehe 27 Disemba mwaka uliopita, Bazoum aliongoza matokeo kwa kupata asilimia 39 ya kura hizo huku Ousmane akimfuata kwa takriban asilimia 17 ya kura.

Mapema Jumanne, waendeshaji kampeni wa Ousmane walidai udanganyifu ulitokea pamoja na wizi na pia visa vya kujazwa kwa masanduku ya kura na vitisho dhidi ya wapiga kura bila kutoa ushahidi.

Rais anayeondoka Mahamadou Issoufou anang’atuka madarakani kwa hiari baada ya kuhudumu mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.

Itakuwa ni mara ya kwanza kwa taifa hilo kushuhudia kupokezana madaraka kati ya viongozi wawili waliochaguliwa tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo 1960.

Taifa hilo limeshuhudia mashambulizi kutoka kwa makundi ya kigaidi yaliyojihami kutoka nchi jirani za Mali na Nigeria.

Siku ya marudio ya kura hizo, maafisa saba wa tume ya CENI waliaga dunia baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa ardhini Magharibi mwa eneo la Tillaberi.