Categories
Michezo

Wachezaji wa Kenya waripoti kambini kujiandaa kwa michezo ya Olimpiki

Timu ya Kenya kwa michezo ya Olimpiki mwaka huu mjini Tokyo Japan imeingia kwenye kambi ya mazoezi katika kambi ya mazoezi uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Timu zilizoripoti kambini ni pamoja na ile ya riadha na zitafuatwa na zile za Voliboli na raga.

Kulingana na kamati ya Olimpiki ya Kenya timu zitafanya mazoezi kwa zamu kutokana na masharti ya kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC ambayo hayarushusu timu nyingi kuwa pamoja.

Wanariadha hao pia watafanyiwa vipimo vya Covid 19 kabla ya kuruhusiwa kwenye hoteli ya Kasarani ambapo baada ya matokeo wataingia kwenye hoteli ya watu wawiliwawili .

Chama cha riadha Kenya kilituma wanariadha 33 katika mita 100 wanaume na wanawake,200 wanaume na wanawake,mita 400 wanaume na wanawake kilomita 20 matembezi wanaume na urushaji sagai watakaoandamana na makocha wao,mameneja na benchi ya kiufundi.

Kulingana na meneja mkuu wa Kenya Waithaka Kioni timu za wachezaji raga 7 kila upande zitakuwa za pili kuripoti kambini baadae wiki hii baada ya kuwasili kutoka Uhispania .

Categories
Michezo

AFCON U 20 kuingia semi fainali Jumatatu

Mashindano ya kuwania kombe la AFCON kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 yatarejelewa Jumatatu usiku kwa mechi za nusu fainali nchini Mauritania.

Ghana watashuka uwanjani dhidi ya Gambia kwa mechi ya kwanza ya nusu fainali saa moja usiku ikiwa marudio baada ya Gambia kuwashinda Ghana mabao 2-1 katika mechi ya kundi C na sasa itakuwa aidha mchuano wa kulipiza kisasi au kudhihirisha ubabe.

Gambia iliibuka ya pili kundi C kwa alama 4 nyuma ya viongozi Moroko wakishindwa na Moroko bao 1-0,kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Tanzania .

Upande wa pili wa sarafu Ghana ukipenda black satelites iliibuka ya tatu kundi C ikiichabanga Tanzania 4-0 kabla ya kutoka sarea tasa dhidi ya Moroko na kupoteza kwa Gambia 1-2.

Nusu fainali ya pili itapigwa saa nne usiku ikiwa baina ya limbukeni na mabingwa wa CECAFA uganda dhidi ya Tunisia mjini Nouakchott.

Uganda maarufu kama Hippos waliizaba Msumbiji magoli 2-0 kabla ya kulimwa na Cameroon 0-1 na kuwabwaga wenyeji Mauriritania 2-1 na kumaliza kwa pointi 6 katika kundi A.

Tunisia ilitoka sare tasa na Burkina Faso katika kundi B kwa alama 4 ,ikitoka sare tasa na Burkina Faso kabla ya kuipiga Namibia 2-0 na kushindwa Afrika ya kati 1-2.

Categories
Michezo

Shujaa na Lionesses zamaliza nafasi za Pili Madrid 7’s

Timu za Kenya kwa wachezaji 7 upande ,Shujaa na Lionesses zilimaliza katika nafasi za pili katika wiki ya pili ya mashindano ya Madrid 7’s yaliyokamilika Jumapili usiku.

Shujaa ilipoteza pointi 7-45 dhidi ya Argentina kwenye fainali ya kombe kuu wakati Lionesses ikiangushwa na Russia alama  19-0 pia kwenye fainali.

Ilikuwa mechi ya nne mtawalia kwa Shujaa kushindwa na Argentina waliokuwa wakiongoza pointi 26 -0 kufikia mapumzikoni huku Vincent Onyala akiifungia Kenya Try ya pekee kipindi cha pili naye  Daniel Taabu akapiga conversion.

Shujaa na Lionesses zilitumia mashindano hayo kujitayarisha kwa michezo ya Olimpiki ziara iliyofadhiliwa na wizara ya michezo.

Matokeo ya Shujaa
Shujaa 26 – Portugal 12
Shujaa 29 – USA 12
Spain 17 – Shujaa 19
28th February
Chile 5 – Shujaa 15
Argentina 36 – Shujaa 19

Cup Final:Shujaa 7 – Argentina 45

Matokeo ya Lionesses
Russia 17 – Lionesses 5
Lionesses 22 – Spain 0
28th February
Lionesses 10 – Poland 12

Cup Final:Lionesses 0 – Russia 19

Categories
Uncategorised

Shujaa na Lionesses wanyakua nafasi za pili Madrid 7’s

Timu ya raga ya wanaume 7 upande Shujaa na  wenzao wa kike Lionesses zilinyakua nafasi za pili katika mashindano ya mwaliko ya Madrid 7’s yaliyokamilika Jumapili usiku nchini Uhispania baada ya kushindwa na Argentina na Urusi mtawalia kwenye fainali za kombe kuu.

Shujaa ilipoteza kwa mara ya nne kwa Argentina kwenye mashindano hayo ya wiki mbili walipochakazwa pointi 7-45 katika fainali ya kombe kuu.

Argentina walianza kwa kasi huku wakiongoza kipindi cha kwanza alama 26 -0 kufikia mapumzikoni huku Shujaa wakionekana kuzidiwa maarifa lakini Vincent Onyala akakomboa try moja kwa Kenya naye Daniel Taabu akapiga Conversion,lakini haikutosha huku Argentina wakiendelea kuongeza tries na  wakaibuka na ushindi wa alama 45-7 kufikia kipenga cha mwisho.

Awali Jumapili Kenya ilikuwa imeshindwa na Argentina pointi 19-36 na kwa jumla walishindwa mara nne kwenye mashindano hayo na timu hiyo ya Amerika Kusini katika kipindi cha wiki mbili.

Matokeo ya Shujaa katika wiki ya pili ya Madrid 7’s

FT: Kenya 26-12 Portugal,
FT: Kenya 29-12 USA,
FT: Kenya 19-17 Spain,
FT: Kenya 15-05 Chile,
FT: Kenya 19-36 Argentina,
FT: Kenya 07-45 Argentina (CUP FINAL),

Timu ya wanawake ya Lionesses pia ilishindwa na Russia katika fainali ya kombe kuu waliponyukwa alama 19-00 na Russia kwenye fainali ya kombe kuu.


Awali pia Lionnesses walicharazwa alama 17-5 na Urusi mapema Jumapili.

Matokeo kamili ya wiki ya pili kwa Lionnesses

FT: Kenya 05-17 Russia,
FT: Kenya 22-00 Spain,
FT: Kenya 10-12 Poland,
FT: Kenya 00-19 Russia (CUP FINAL)

Shujaa na Lionesses walitumia mashindano hayo ya mwaliko kujiandaa kwa michezo ya Olimpiki baina ya Julai na Agosti mwaka huu mjini Tokyo Japan.

Categories
Michezo

Timu ya mbio za nyika ya Kenya kuvunja kambi Jumatatu

Wanariadha 46 na maafisa 10 ambao wamekuwa kwenye kambi ya mazoezi katika chuo cha mafunzo ya walimu cha Kigari TTC kaunti ya Embu wanatarajiwa kuvunja kambi Jumatatu kurejea makwao baada ya kuahirishwa kwa makala ya 6 ya mashindano ya mbio za nyika barani Afrika yaliyokuwa yaandaliwe Lome Togo kati ya tarehe 6 na 7 mwezi huu.

Togo ilitangaza wiki iliyopita kujiondoa kuandaa mashindano hayo ya Afrika kwa kuhofia msambao wa Covid 19 na kuliacha shirikisho la riadha Afrika kwenye njia panda kutafuta waandalizi wapya.

Hata hivyo chama cha riadha Kenya kilitangaza kuwa wanariadha waliokuwa kambini Embu wasalie, huku wakisubiri hatima ya mwandalizi mpya.

Kwa yamkini hakuna mwandalizi ambaye atapatikana kwa dharura na hivyo basi mashindano hayo yamefutiliwa mbali baada ya kuahirishwa pia mwaka jana kutokana na uchaguzi mkuu nchini Togo.

Categories
Michezo

Lioness kuvaana na Russia huku Shujaa ikikabana koo na Argentina Fainali ya Madrid 7’s

Timu ya Kenya ya raga kwa wachezaji 7 kila upande maarufu kama lionesses watarejea uwanjani Madrid kuanzia saa moja usiku wa Jumapili kwa fainali ya kombe kuu dhidi ya Russia.

Fainali ya kombe kuu kwa wanaume itafuatia saa moja unusu usiku Kenya Shujaa wakijaribu kuishinda Argentina kwa mara ya kwanza baada ya kupoteza mara tatu kwa wapinzani hao ikiwemo jumapili adhuhuri.

Categories
Michezo

Vipusa wa KCB watoka nyuma na kutoboa mabomba ya Kenya Pipeline ligi kuu Voliboli

Vigogo KCB walistahimili ukinzani mkali kabla ya kutoka nyuma na kuichara Kenya Pipeline seti 3-1 katika mechi ya kusisimua ya ligi kuu Voliboli iliyopigwa katika ukumbi wa Nyayo Jumapili alasiri.

Pipeline walianza kwa makeke na na kushinda seti ya kwanza alama 25-23 lakini wanabenki KCB chini ya ukufunzi wa kocha Japheth Munala wakatumia tajriba na kutwaa seti 3 zilizofuatia alama 25-21,25-19 na 25-17.

Naiorbi Prisons wakimenyana na Kenya Prisons

Katika mechi ya mapema Jumapili katika ukumbi huo wa Nyayo Kenya Prisons waliititiga Nairobi Prisons pia seti sawa za 3-1 wakishinda seti mbili za ufunguzi 25-15 na 25-18 kabla ya kupoteza ya tatu 21-15 na kushinda seti mbili za mwisho 25-21 na 29-27.

Categories
Michezo

Ingwe waikwaruza Homeboyz ligi kuu FKF

Miamba wa soka Kenya Afc Leopards walisajili ushindi wa pili mtawalia kwenye ligi kuu FKF chini ya kocha mpya Patrick Auseems kutoka Ubelgiji walipowaadhibu Kakamega Homeboyz magoli 2-1 katika pambano la Jumapili uwanjani Bukhungu ukiwa ushindi wa kwanza kwa Leopards katika uga huo.

Clyde Senaji aliwaweka wageni Ingwe uongozini kwa goli la kwanza dakika ya 10, kabla ya lvis Rupia kuongeza la pili huku wakiongoza 2-0 kufikia mapumzikoni.

Allan Wanga alifunga bao la kufuta machozi kwa wenyeji na mechi kumalizika kwa ushindi wa Leopards 2-1.

Katika michuano mingine Bandari Fc pia walizidisha makali yao kwa kuinyoa Ulinzi Stars mabao 2-0 katika uwanja wa Kericho Green,Sofapaka wakasajili ushindi wa mabao 2-1 ugenini kwa Posta Rangers nao Kariobangi Sharks wakawafilisi KCB kwa kuwazabua mabao 3-0.

Tusker Fc waliolimwa na Bidco United Jumamosi wangali kushikilia kukutu uongozi wa ligi hiyo kw alama 32 baada ya mechi 14,wakifuatwa na KCB kwa pointi 26,pointi moja zaidi Bandari Fc iliyo ya tatu na AFC Leopards katika nafasi ya 4 wakati Kariobangi Sharks wakihitimisha tano boar kwa alama 24.

Categories
Michezo

Shujaa yazidiwa maarifa na Argentina kwa mara tatu Madrid 7’s

Timu ya taifa ya Kenya kwa wachezaji 7 kila upnde imepoteza kwa Argentina pointi 19-36 katika mechi ya mwisho Jumapili alasiri katika mashindano ya Madrid 7’s.

Shujaa chini ya ukufunzi wa Innocent Simiyu ilikuwa nyuma alama 7-24 kufikia mapumzikoni Try ya pekee yaKenya ikifungwa na Bush Mwale kabla ya kujipatia alama nyingine mbili kwa Conversion.

Argentina walitanua uongozi wao hadi alama 7-31,kabla ya Jacob Ojee kupiga try ya pili wakati Daniel Taabu akifunga conversion na kupunguza pointi hadi 14-31, na kisha baadae Ojee akapiga try ya pili huku Taabu akikosa conversion na hadi kipienga cha mwisho Kenya wakapoteza alama 19-36.

Awali Shujaa waliikomoa Chile 15-5 katika mechi ya kwanza na ushinde dhidi ya Argentina ulikuwa wa tatu mtawalia baada pia ya kulemewa na timu hiyo ya Amerika kusini wiki jana.

Matokeo ya Jumamosi Februari 27

FT: Kenya 26-12 Portugal,
FT: Kenya 29-12 USA,
FT: Kenya 19-17 Spain,

Categories
Michezo

Daisy Cherotich na Gideon Rono watamba siku ya pili ya riadha Nyayo

Daisy Cherotich ametwaa ushindi wa mbio za mita 10,000 wanawake katika siku ya pili na ya mwisho ya mashindano ya uwanjani maarufu kama Track and Field yaliyoandaliwa uwanja wa taifa wa Nyayo Jumapili.

Cherotich alizikamilisha mbio hizo kwa dakika 32 sekunde 19 nukta 1 akifuatwa na Everlyn Chirchir kwa dakika 32sekunde 37 nukta 9 huku Joyce Chepkemoi akiridhika katika nafasi ya tatu kwa dakika 32 sekunde 58 nukta 8.

Geideon Rono alimwonyesha kivumbi bingwa wa kitaifa katika mbio nyika Rodgers Kwemoi na kunyakua ushindi katika mita 5000 alipokata utepe kwa dakika 13 sekunde 21 nukta 2 akifuatwa na Kwemoi kwa dakika 13 sekunde 21 nukta 8 huku Daniel Simiu akihitimisha tatu bora kwa dakika 13 sekunde 29 nukta 6.

Lydia Jeruto aliibuka mshindi katika mita 1500 akitumia dakika 4 sekunde 15 nukta 2 akifuatwa na Vivia Kosgei kwa dakika 4 sekunde 15 nukta 7 wakati Esther Wambui akitwaa nafasi ya tatu kwa dakika 4 sekunde 16.

Mashindano hayo ya siku mbili yalipaswa kuandaliwa katika chuo kikuu cha Bondo lakini yakahamishwa hadi Nairobi ,na sasa mkondo wa pili utaandaliwa kati ya Machi 12 na 13 katika kaunti ya Embu ukifuatwa na mkondo wa tatu na wa mwisho mjini Mumias baina ya April 2 na 3 .
Yafuatayo ni baadhi ya matokeo ya Jumapili

10,000m women
1. Daisy Cherotich 32:19.1
2 Everlyn Chirchir 32:37.9
3 Joyce Chepkemoi 32:58.8
4 Gladys Koech 34:17.3
5000m men
1 Gideon Rono 13:21.2
2 Rodgers Kwemoi 13:21.8
3 Daniel Simiu 13:29.6
4 Michael Kibet 13:36.6
5 Stanley Waithaka 13:43.7
1500m women
1 Lydia Jeruto 4:15.2
2 Vivian Kosgei 4:15.7
3 Esther Wambui 4:16.0
4 Loice Chemining 4:16.2
400m women
1 Hellen Syombua 55.17
2 Janet Jepkoech 57.95
3 Mercy Jerop 59.36
4 Faith Moraa 59.30
400m men
1 Zablon Ekwam 45:65
2 William Raiyan 46.13
3 Wycliffe Kinyamal 46.55

Baadae kutaandaliwa majaribio ya kitaifa kati ya tarehe 16 na 17 April katika uwanja wa Nyayo ambapo AK itateua wanariadha watakaoshiriki makala ya 22 ya mashindano ya Afrika nchini Algeria baina ya Juni 1 na 5 mwaka huu.