Atletico Madrid wavunja nuksi ya miaka 10 ya La Liga kwa kuwaparuza Barcelona
Atletico Madrid hatimaye walisajili ushindi wa kwanza wa ligi kuu Uhispania La liga dhidi Barcelona ndani ya miaka 10 iliyopita walipowalaza vijana wa Katalunya bao 1-0 katika uwanja wa Wanda Metropolitano Jumamosi usiku.
Madrid chini ya Meneja Diego Simeone walifahamu fika kuwa ushindi ungewachupisha hadi nafasi ya kwanza ligini sawia na Real Sociadad na walianza pambano hilo kwa makeke na mashambulizi makali ingawa Barca pia walikaa ange na kuashiria huenda kipindi cha kwanza kingekamilika kwa sare tasa.
Lakini utepetevu na uzembe wa kipa wa Barcelona Andre Tes Tegen wa kuchomoka langoni kunako dakika ya 3 ya muda wa mazidadi katika kipindi cha kwanza ukampa mshambulizi Yanick Carasco fursa ya kufunga bao rahisi na likadumu hadi kipenga cha mwisho .
Ulikuwa ushindi wa kwanza wa Madrid dhidi ya Barca katika ligi kuu baada ya kujaribu mara 20 bila mafanikio.
Kwa upande mwingine kipigo hicho kiliwaacha Barca wanaonolewa na mwalimu Ronald Koeman katika nafasi ya 10 kwa point 11 baada ya mechi 8 huku pia wakiwapoteza wanandinga wakiwemo beki kisiki Gerard Pique na Sergi Roberto kwa majeraha ,na kuongeza kwa orodha ndefu ya majeruhi ikiongozwa na Ansu Fati atakayesalia nje kwa miezi miezi minne ijayo.
Atletico Madrid wanaongoza Jedwali kwa pointi 20 sawia na Sociadad huku mabingwa watetzi Real Madrid wakizoa alama 17 katika nafasi ya nne baada ya kutoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Villareal iliyo ya tatu Jumamosi jioni.