Askofu Njue akashifu tabia za viongozi nchini

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki John Cardinal Njue amekashifu vikali matamshi ya uchochezi yanayotolewa na viongozi wa kisiasa yanayosababisha utengano miongoni mwa Wakenya.

Akizungumza katika Kanisa la Holy Family Basilica Jijini Nairobi wakati wa misa takatifu iliyopeperushwa na Runiga ya KBC Channel 1, Njue amesema kuwa tabia ya viongozi hao inaonyesha mfano mbaya katika nchi hii.

“Nchi yetu iko na shida, tuwaombee viongozi wetu,” amesema askofu huyo.

Haya yanajiri siku moja baada ya kuachiliwa huru kwa Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ambaye alikamatwa na kushtakiwa kwa matamshi ya chuki dhidi ya aliyekuwa mama wa taifa wa kwanza Ngina Kenyatta.

Wakati uo huo, Askofu Njue ameadhimisha miaka 34 tangu alipokuwa kasisi, akisema kuwa safari yake ya uhubiri imekuwa yenye changamoto nyingi.

Njue alikuwa kasisi wa kwanza wa kanisa Katoliki tawi la Embu mwaka wa 1986 baada ya kuteuliwa na Papa John Paul wa pili.

“Nilipoteuliwa kama kasisi wa kwanza huko Embu, tulikuwa hatuna nyumba ya kuishi na maisha yalikuwa magumu sana. Nilimuamini Mungu katika safari yangu kwa sababu ndiye aliyenituma kuifanya kazi yake. Mungu alinipa nguvu za kumtumikia kikamilifu,” amesema Askofu Njue.

Kwa miaka mingi, Askofu huyo ametoa wito wa utulivu na amani nchini, kila mara akihubiri ujumbe wa upendo na umoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *