Ashanti azuru Kenya

Mwanamuziki wa Marekani Ashanti kwa jina halisi Ashanti Shequoiya Douglas ameonekana nchini Kenya hususan jijini Nairobi na inaaminika amekuja kwa likizo.

Mwanadada huyo wa miaka 40 aliweka video fupi kwenye Instagram sehemu ya ‘stories’ ambayo ilimwonyesha akiwa kwenye kijigari kidogo akipelekwa kwenye chumba cha kulala katika hoteli ya kifahari ambayo hakuitaja lakini alisema yuko Nairobi.

Nyingine inamwonyesha akifurahikia chumba chake cha kulala kwenye hoteli hiyo.

Ujio wake haujajulikanishwa na waandalizi wa tamasha nchini na inadhaniwa kwamba hajakuja kikazi kama mwanamuziki bali amekuja tu kuzuru nchi ya Kenya.

Haijulikani mwanamuziki huyo ambaye alivuma sana mwaka 2002 atakuwa nchini Kenya kwa muda gani. Mwaka huo wa 2002 alishirikishwa na mwanamuziki Fat Joe kwenye kibao “What’s Love?” ambacho kilivuma sana na akashirikishwa pia na Ja Rule kwenye kibao “Always on Time”.

Alianza kazi ya muziki akiwa kijana na baadaye akawa mwanamke wa kwanza kuwahi kushikilia nafasi mbili za kwanza kwenye shindano la muziki kwa jina “Billboard Hot 100” pale ambapo nyimbo zake za ‘Foolish’ na ‘What’s Love’ zilishikilia nafasi za kwanza na pili mtawalia.

Yeye hujihusisha pia na maswala ya mitindo ya mavazi na uigizaji.

Jina lake “Ashanti” linatokana na ufalme uliokuwepo kitambo Barani Afrika katika sehemu ambayo sasa ni nchi ya Ghana ambao watu wengine waliuita “Asante”. Katika ufalme huo, wanawake walikuwa na uwezo mkubwa na ushawishi na mamake mwanamuziki huyu alitaka awe hivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *