Ardhi yahusishwa na changamoto za usalama hapa nchini

Asilimia 25 ya changamoto zote za usalama humu nchini zinahusiana moja kwa moja na Ardhi.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa mpango wa miaka mitano wa utendaji kazi ya Tume ya kitaifa ya ardhi,waziri wa usalama wa kitaifa,Dkt Fred Matiang’i alitaja mizozo ya umiliki wa ardhi, kughushi hati za kumiliki mashamba, utapeli wa ardhi na unyakuzi wa ardhi miongoni mwa masuala mengine kuwa changamoto kubwa kwa usalama humu nchini.

Alisema masuala ya kufidia ardhi kama ile ya ujenzi wa reli ya kisasa ndizo baadhi ya changamoto kubwa zaidi za utekelezaji wa miradi ya ajenda nne kuu za maendeleo.

Aliipongeza tume ya kitaifa ya ardhi kwa kushughulikia suala hilo.

Aliihimiza tume hiyo ihakikishe taasisi za serikali zina stakabadhi za kumiliki ardhi ili kuepusha mizozo ya umiliki wa ardhi.

Mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya umiliki wa ardhi Gershom Otachi alisema tume yake itashauriana na wadau wote wa sekta ya ardhi ili kushughulikia mizozo ya ardhi katika viwango vya kitaifa na vya kaunty.

Mpango huo wa utenda kazi unatarajiwa kutoa mwongozo kwa tume hiyo wa kutekeleza majukumu yake kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *