Anne Kansiime atangaza kwamba anatarajia mtoto

Mchekeshaji wa nchi ya Uganda Anne Kansiime ametangaza kwamba yeye na mpenzi wake Abraham Tukahiirwa ambaye ni mwanamuziki, wanatarajia mtoto wao wa kwanza.

Kwenye akaunti yake ya Instagram Kansiime alipachika picha yake ambayo inaonyesha ujauzito wake akisema kwamba ametafuta njia ya kuambia mashabiki wake kuhusu habari hiyo njema kwa muda sasa.

Aliahidi pia kutumbuiza mashabiki wake kesho Ijumaa tarehe 16 mwezi Aprili mwaka 2021 baada ya kuwakosa kwa muda mrefu.

Onyesho lake litakuwa moja kwa moja kwenye You Tube na anashirikiana na jarida la “The Pulse Uganda”. Mchekeshaji huyo anasema ana mengi kwa mashabiki wake na hajui ataanzia wapi.

Anne ambaye wengi humrejelea kama malkia wa uchekeshaji barani Afrika, aliwahi kuolewa na Gerald Ojok kwa muda wa miaka mitano kati ya mwaka 2013 na 2017.

Ndoa hiyo ilivunjika lakini habari kuhusu hayo zilijiri miezi sita baadaye huku mwanadada huyo akifichua kwamba alijitolea mahari ili kumwezesha Ojok kumwoa.

Muigizaji huyo wa kipindi cha MiniBuzz alisema pia kwamba aliharakisha kuingia kwenye ndoa na ndio sababu kuu iliyosababisha kuvunjika kwake. Kulingana naye, alikuwa na mpango wa maisha ambao alifuata bila hata kufikiria kwa makini. Alipanga asome, apate kazi na apate mume afunge ndoa.

Karibu mwaka mmoja baada ya ndoa hiyo kuvunjika, Kansiime aliingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na Skylanta au ukipenda Abraham Tukahiirwa lakini hawajawahi kusema lolote kuhusu kufunga ndoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *