Categories
Habari

ANC chapongeza Jubilee kwa kujiondoa kwenye uchaguzi mdogo wa Matungu

Chama cha Amani National Congress (ANC) kimesifu hatua ya kile cha Jubilee ya kutodhamini mgombea katika uchaguzi mdogo wa Eneo Bunge la Matungu.

Kwenye taarifa, chama hicho kimesema kuwa chama cha Jubilee kitamuunga mkono mgombea wa ANC Oscar Nabulindo katika uchaguzi huo.

“Chama cha Jubilee kimetangaza leo kwamba kimeamua kumuunga mkono mgombea wa ANC Peter Oscar Nabulindo katika uchaguzi mdogo wa tarehe nne mwezi Machi, 2021 katika Eneo Bunge la Matungu,” kimesema chama hicho.

Chama hicho cha ANC, chake Musalia Mudavadi, kimeahidi kuhamasisha wakazi wa eneo bunge hilo ili kumtafutia Nabulindo umaarufu katika uchaguzi huo mdogo.

Haya yanafuatia tangazo la chama cha Jubilee kwamba hakitadhamini wagombeaji katika chaguzi ndogo tatu za Eneo Bunge la Matungu, lile la Kabuchai na kiti cha Useneta wa Kaunti ya Machakos kufuatia vifo vya waliokuwa viongozi wa sehemu hizo.

Akitaarifu waandishi wa habari baada ya kikao cha mashauriano na viongozi wa chama hicho kwenye Bunge la Kitaifa na Seneti, Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju amesema uamuzi huo unaambatana na moyo wa kuhimiza maridhiano wa kuruhusu vyama tanzu vya mseto wa NASA kudhamini wagombeaji kwenye chaguzi hizo mdogo.

Hata hivyo, Tuju amedokeza kuwa chama cha Jubilee kitakuwa na wagombeaji kwenye kinyang’anyiro cha Ugavana wa Nairobi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *