Amber Rose afunza mwana wa kiume wa miaka 7 kuhusu hedhi

Mwanamitindo na muigizaji wa Marekani Amber Rose amezua maswali chungu nzima baada ya kufichua jinsi analea watoto wake.

Amber alikuwa akizungumza kwenye kipindi cha mahojiano almaarufu “Red Table Talk’ ambacho huendeshwa na Jada Pinkett Smith, mamake Adrienne Banfield-Norris na binti yake Willow Smith.

Alikiri kwamba kifungua mimba wake wa miaka saba kwa jina Sebastien tayari anajua kuhusu hedhi na jinsi ya kuhusiana na watoto wa jinsia ya kike kwa heshima.

“Nikiwa nimeketi Sebastien atakuja karibu aniulize kama naumwa, kama nina hedhi, kama ninahitaji sodo na mengine.” Alisema Amber.

Maneno hayo yalionekana kumshangaza sana mamake Jada ambaye alikodoa macho na Amber akaendelea kuelezea, “Nataka akitimiza miaka 13 na wasichana wa darasa lake wakipata hedhi anawasaidia wakati wavulana wengine labda watatoroka.”

Baada ya hapo mama huyo alimpongeza Amber Rose kwa njia nzuri ambayo analea watoto wake.

Kwa muda wa miaka mingi, Bi. Amber amejulikana kama mtetezi wa haki za wanawake na mara nyingi amesikika akisema anataka watoto wake ambao ni wa kiume wakue wakiwa watetezi wa wanawake.

Mwanamitindo huyo alisema pia kwamba anafunza watoto wake kuhusu mipaka na watoto wengine na pia kufanya mambo kwa idhini ya wengine.

“Nina michoro mingi kwa nyumba yangu ambayo inahimiza utetezi wa wanawake, mingine ni ya wanawake ambao wako uchi na mwanangu amezoea.” Aliongeza Amber.

Muigizaji huyu wa marekani anasema aliamua kulea watoto wake kwa njia hiyo maanake wakati akikua ilikuwa mwiko kuzungumzia mambo kama hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *