Amanda Gorman kwenye Jalada la Jarida la Vogue!

Amanda Gorman alipata umaarufu ulimwenguni kote baada ya kukariri shairi lenye mada “The Hill We Climb” kwenye sherehe ya uapisho wa Rais Joe Biden wa Marekani tarehe 20 mwezi Januari mwaka huu wa 2021.

Yeye ndiye wa umri mdogo zaidi kati ya washairi wote ambao wamewahi kutumbuiza kwenye sherehe za kuapishwa kwa Marais nchini Marekani.

Mwanadada huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 23 ndiye atakuwa kwenye jalada la toleo la mwezi Mei la jarida la Vogue jambo ambalo alitangaza kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Gorman ni mwingi wa furaha akisema amehisi ameheshimiwa zaidi kwa kuwa mshairi wa kwanza kuwa kwenye jalada la Vogue, jarida ambalo huangazia mitindo ya mavazi na ya maisha.

Nakala ya jalada hilo ilitolewa na Vogue jana Jumatano.

Bi. Amanda alielezea kwamba kwenye picha hizo, amevaa mavazi yaliyoundwa na mwanamitindo mweusi aitwaye Virgil Abloh.

Abloh pia ni mpiga muziki au ukipenda DJ na ndiye huelekeza mitindo ya mavazi kwa wanaume chini ya nembo ya Louis Vuitton.

“Huku ni kuinuka kwa Amanda Gorman, lakini pia ni kuinuka kwa wote ambao huwa ninataja na wasioonekana ambao huniinua kila wakati, ninawapenda.” aliongeza kusema Amanda.

Kazi ya ushairi imesababisha msichana huyo ambaye alikuwa na tatizo la kushindwa kuzungumza akiwa mdogo atagusane na watu kadhaa maarufu nchini Marekani.

Aliwahi kuhojiwa na Oprah Winfey ambaye alimzawadi pete na hereni ambavyo alivaa kwenye sherehe ya kuapishwa kwa rais Joe Biden.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *