Alexei Navalny atakiwa kurejea Russia mara moja
Huduma ya magereza nchini Russia siku ya Jumatatu ilikabidhi serikali agizo la kumtaka Alexei Navalny ,ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali kurejea mjini Moscow Jumanne asubuhi mara moja kutoka Ujerumani ambako alikwenda kwa matibabu.
Taarifa hiyo imesema asipotimiza makataa hayo,atatiwa nguvuni na kufungwa atakaporejea nchini humo.
Navalny,ambaye ni mkosoaji wa utawala wa Rais Vladmir Putin alipelekwa kwa ndege hadi Ujerumani kupokea matibabu mwezi Agosti mwaka jana baada ya kuanguka ghafla kwenye ndege moja katika kile ambacho Ujerumani na mataifa ya magharibi yalisema lilikuwa jaribio la kutaka kumuua kwa gesi ya sumu ya Novichok.
Hata hivyo Russia imesema hakuna ushahidi wowote kuhusu madai hayo na kukanusha kuhusika katika kisa hicho.
Huduma ya magereza ya taifa hilo siku ya jumatatu ilimshutumu Navalny kwa kuvunja sheria kuhusu kuahahirishwa kifungo chake anachotumikia akiwa nje.
Alihukumiwa kifungo cha nje mwaka wa 2014 kwa kosa la kukwepa sheria za halmashauri kuhusu uhalifu.