Akon aingilia biashara ya madini nchini Congo

Mwanamuziki wa Marekani wa mtindo wa R&B Aliaune Damala Badara Akon Thiam maarufu kama Akon ameingilia biashara ya kuchimba madini katika nchi ya Congo.

Kampuni yake imeingia kwenye mkataba na kampuni ya serikali ya Congo ya kuchimba madini – Sodimico, ambapo atatoa usaidizi wa kifedha katika eneo moja la kuchimba madini.

Mwanamuziki huyo ambaye ana asili ya Senegal barani Afrika amekuwa akijihusisha na biashara tofauti na mipango ya usaidizi barani Afrika kwa miaka ya hivi karibuni.

Anajenga jiji lake nchini Senegal kwa gharama ya dola bilioni sita za marekani na anamiliki biashara ya hela kwa jina Akoin.

Kampuni anayosimamia Akon iliyosajiliwa nchini Marekani ‘White Waterfall LLC’ imekubaliana na serikali ya Congo, kutoa dola milioni mbili za Marekani ambazo zitatumika katika kuendesha shughuli kwenye sehemu ya kuchimba madini inayoitwa Kimono katika mkoa wa Haut Katanga nchini Congo.

Nchi ya Congo ndiyo inaongoza kwa uzalishaji wa madini ya Copper barani Afrika na inaongoza kwa uzalishaji wa madini ya Cobalt ulimwenguni.

Cobalt hutumika kuunda betri za gari.

Kulingana na maelezo kwenye tovuti yake, kampuni ya White Waterfall LLC huwekeza kwenye kampuni za kuchimba madini lakini hakujatolewa orodha ya kampuni ambazo imewahi kushirikiana nazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *