AK yaendeleza matayarisho ya mbio za nyika za kitaifa Februari 13 baada ya kaunti ya Kisii kujiondoa
Chama cha riadha Kenya kinakaribia kukamilisha maandalizi ya majaribio ya kitaifa ya mbio za Nyika tarehe 13 mwezi huu katika uwanja wa Ngong Race Course baada ya kaunti ya Kisii kushindwa kuandaa mashindano hayo.
Kulingana na afisa wa baraza kuu la Athletics Kenya Barnaba Korir, chama cha AK South Nyanza kilijiondoa kuandaa mashindano hayo baada ya kaunti ya Kisii kudinda kutoa ufadhili.
“Unajua hii ni mara ya pili kwa hii region kushindwa kuandaa mashindano ya kitaifa ,Ilibidi tuhamishe mashindano hayo kutoka Kisii baada ya mwenyekiti wa Ak South Nyanza kutuandikia barua akisema kuwa hawana uwezo wa kuandaa mashindano kufuatia hatua ya kaunti ya Kisii kukataa kutoa ufadhili,sasa tayari tumeanza matayarisho ”
Korir amesisitiza kuwa kwenda mbele itabidi kaunti zinazonuia kuandaa mashindano hayo kusaini mkataba na afisi kuu ya AK ili kusitokee mkanganyiko.
“Kwenda mbele itabidi kaunti zote zinazonuia kuanda mashindano ya kitaifa kusaini mkataba wa makubaliano na afisi kuu ya AK ili kusiwe na hali kama hii,kwa sasa chama cha riadha kinaendelea na matayarisho ingawa pia tunahimiza serikali za kaunti kutenga kiwango cha pesa kwa michezo ya kitaifa”akaongeza Korir
Hata hivyo AK imesisitiza kuwa wanariadha watakaoruhusiwa kushiriki mashindano ya kitaifa ni wale wanaotokea katika matawi ya AK ambayo lazima yawe yameandaa mashindano yao.
“Wanariadha watakaoshiriki ni wale tu wanaowakilisha tawi la chama hicho bali sio wanariadha wa kibinafsi”akasema Korir
Mashindano ya kitaifa ya kukata mbuga yataandaliwa Februari 13 ambapo chama cha AK kitateua timu itakayoshiriki mashindano ya mbio za nyika barani Afrika kati ya Machi 6 na 7 mjini Lome Togo.