Ajuma Nasenyana asherehekea siku ya kuzaliwa ya mwanawe

Kwa njia ya kipekee mwanamintindo huyo wa kimataifa mwenye asili ya Kenya amesherehekea kuzaliwa kwa mtoto wake wa kwanza amabye anatimiza umri wa miaka kumi sasa.

Amewavunja mbavu wafuasi wake pale aliposimulia vituko ambavyo alikuwa akivifanya kwenye wadi ya kujifungulia kina mama kwenye hospitali moja huko Uswidi wakati akitarajia huyo mtoto wake.

Kwenye akaunti yake ya Instagram, Ajuma alipachika picha ya mtoto huyo wa kiume kwa jina Elliot na kuandika, ” Hebu fikiria mwanamke mrefu mjamzito wa jamii ya Turkana akikimbia kwenye wadi ya kujifungulia kina mama na wauguzi wa Uswidi, madaktari na mtaalamu wa kujifungua wakimkimbiza. Ndiyo hadithi yangu wakati nikijifungua huyu mvulana. Kila mara nilipozidiwa na uchungu nilisimama na kukimbia. Sijui ni vipi lakini kukimbia huko kulinituliza ilhali hicho kilikuwa kionjo tu cha uwazimu wangu wa uchungu wa kujifungua. Ninaweza kukubali kupitia uchungu kila mara kwa ajili ya huyo mtoto mkarimu. Nisaidieni kutakia kifungua mimba wangu mema anaposherehekea siku yake ya kuzaliwa.”

Ajuma Nasenyana ambaye ana umri wa miaka 36 sasa ni mwanamitindo ambaye amefanya kazi na kampuni kadhaa za kimataifa za kuunda na kuuza mavazi na za bidhaa za urembo.

Alizaliwa katika eneo la Lodwar nchini Kenya na aliingilia kazi hiyo ya uanamitindo kupitia shindano la ulimbwende kwa jina “Miss Tourism Kenya” mwaka 2003, ambapo alivikwa taji ya “Miss Nairobi”.

Baadaye alichukuliwa na Sarazuri Modeling Agency yake Lyndsey McIntyre.

Wakati kampuni ya kupiga picha ya Gamma ilizuru Kenya kuangazia jinsi McIntyre alikuwa akiendesha kazi ya kusaka wanamitindo ilivutiwa sana na Ajuma na akawa mhusika mkuu kwenye makala yao.

Picha zake zilisambazwa kwenye majukwaa kadhaa ya kimataifa na mwaka huo wa 2003, Nasanyana alisafiri kuelekea uingereza ambapo aliingia kwenye mikataba na kampuni nyingi za London, Italy, Austria, Spain, Ireland, Canada na Sweden.

Ajuma ana ngozi ya rangi nyeusi na alikuwa na dhamira ya kuzindua bidhaa za urembo kwa ajili ya wanawake ambao wana rangi sawa na yake katika kujaribu kukabiliana na shinikizo za sasa za wanawake weusi kujichubua ili wakubalike katika jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *