Ajali ya treni yasabaisha lita 750,000 za mafuta ya mawese kumwagika mto Kambu

Halmashauri ya maji imewatahadharisha watu wanaoishi kando-kando ya mto Kambu,Kaunti ya Makueni wasiyatumie maji ya mto huo baada ya treni kumwaga lita alfu 750 za mafuta ya mawese kwenye eneo hilo.

Maji ya mto huo ambayo huelekea mtoni Athi hutegemewa mno na wakazi wa eneo hilo kwa matumizi ya nyumbani na unyunyiziaji maji mashambani.

Halmashauri hiyo imetoa ilani hiyo kwa wakazi katika sehemu maalum na katika vituo vya kibiashara, siku mbili baada ya ajali hiyo ya treni katika reli ya zamani.

Mwenyekiti wa kamati ya mazingira katika bunge la Kaunti ya Makueni, Joseph Muema na afisa mkuu anayesimamia mazingira Mary Mbenge, walionya kuwa mafuta hayo yana madhara mengi kwa mazingira.

Maafisa hao wametoa wito kwa shirika la reli humu nchini kulinda sehemu yalikomwagika mafuta hayo huku wakionya wakazi dhidi ya kuyatumia mafuta hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *