Categories
Michezo

Ahly waipiga kumbo Wydad na kutinga fainali ya 9 ya Ligi ya Mabingwa Caf

Mabingwa mara 8   ligi ya mabingwa Afrika Al Ahly ya Misri walitinga fainali ya taji hiyo kwa mara ya 9 baada ya kuwacharaza Wydad Casablanca ya Moroko mabao 3-1 katika marudio ya nusu fainali jijini Cairo Ijumaa Usiku.

Marwan Mohsen na  Hussein Elshahat walipachika mabao ya Ahly maarufu kama Red Devils walioenda mapumzikoni kwa ushindi wa mabao 2 -0, kabla ya Yasser Ahmed Ibrahim kuongeza bao la tatu kunako kipindi cha pili kupitia kichwa , naye nguvu mpya  Zouheir El Moutaraji akifunga bao la maliwazo kwa wageni.

Ahly wanaofunzwa na kocha Pitso Mosimane kutoka Afrika kusini walifuzu kwa fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1 ,baada ya kusajili ushindi wa mabao 2-0 katika duru ya kwanza ya nusu fainali wiki jana.

Itakuwa mara ya tisa kwa miamba hao wa Misri kucheza fainali ya kombe hilo la kifahari barani Afrika ,wakijivunia rekodi ya kutoshindwa katika mechi 28 za ligi ya mabingwa Afrika na ushindi wa 17 mtawalia nyumbani  .

Ahly watakuwa wakiwania kombe hilo kwa mara ya 9  wakiwa na rekodi ya kutopoteza katika fainali na pia wakiwania kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2013, huku kocha Mosimane akiwinda kombe la pili  la ligi ya mabingwa Afrika baada ya kulinyakua miaka 4 iliyopita akiwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Mabingwa wa Misry Al Ahly watukatana kwenye fainali ya Novemba 6 na mshindi wa nusu fainali ya pili baina ya Zamalek ya Misri dhidi ya mabingwa wa Moroko Raja Casablanca ambayo iliahirishwa kutoka Oktoba 24 baada ya wachezaji  8 wa Casablanca kupatikana na Covid 19.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *