Ahly na Zamalek kuzindua uhasama wa jadi fainali ya ligi mabingwa Ijumaa
Fainali ya ligi ya mabingwa barani afrika itasakatwa Ijumaa usiku katika uwanja wa Cairo International ,ikiwa derby ya Cairo baina ya mabingwa mara 8 Al Ahly dhidi ya Zamalek kuanzia saa nne usiku.
Timu hizo zitakutana kwa mara ya 9 katika kombe hilo la ligi ya mabingwa, Ahly wakiibuka washindi mara 5 na nyingine 3 kuishia sare, lakini zote zikiwa aidha mechi za makundi au nusu fainali.
Itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika fainali ya kombe hilo zikiwania dola milioni 2 nukta 5 na fursa ya kucheza kombe la dunia baina ya vilabu.
Katika mechi za nyumbani timu hizo zimepambana mara 215 Ahly maarufu kama Red Devils wakishinda mechi 91 ,huku Zamalek wajulikanao kama White Knights wakisajili ushindi kwenye michuano 50 na kurekodi sare 74 .
Ahly wamenyakua ligi ya mabingwa mara 8 ikiwa timu iliyoshinda taji hiyo mara nyingi zaidi na kushinda mataji 4 ya kombe la shirikisho,4 ya African Cup winners cup na lile la super cup mara 4 kwa jumla wakiwa na vikombe 19 vya Afrika.
Hata hivyo Red Devils wamekawia tangu mwaka 2014 ikiwa mara ya mwisho kwao kunyakua kombe la shirikisho huku yale ya ligi ya mabingwa yakiwakwepa na ndiyo timu iliyokawia muda mrefu zaidi kabla ya kushinda kombe la ligi ya mabingwa.

Upande wa pili wa sarafu Zamalek wamewshinda mataji matano ya ligi ya mabingwa ,4 ya Super Cup na moja ya shirikisho na nyingine moja ya African cup winners cup wakiwa na vikombe 11 vya Afrika.
Zamalek iliibuka ya pili katika kundi A nyuma ya Toupiza Mazembe kabla ya kuwatema waliokuwa mabingwa matetezi Esperance ya Tunisia jumla ya mabao 3-2 katika robo fainali na kuwabandua Raja Casablanca jumla ya mabao 4-1 kwenye nusu fainali.
Ahly nao waliibuka wapili kundini B nyuma ya Etoile du Sahel kabla ya kuibwaga Mamelodi Sundowns magoli 2-1 katika kwota fainali na hatimaye kuwadhalilisha mabingwa wa Moroko Wydad Casblanca kwa kuwalabua mabao 5-1 katika nusu fainali.
Kocha wa Afrika Kusini Pitso Mosimane alishika hatamu za kuwanoa Ahly mwezi Septemba mwaka huu akitokea Mamelodi Sundowns ya nyumbani ambao alishinda nao kombe hilo la ligi ya mabingwa mara moja .
Jaime Pacheco wa kutoka Ureno alirejea kuwafunza Zamalek pia mwezi Septemba mwaka huu akiwa hana kazi tangu aigure timu hiyo mwaka 2014.

Misri itanyakua kombe hilo la ligi ya mabingwa Ijumaa usiku kwa mara ya 15 likiwa taifa pekee kunyakua mataji mengi zaidi kwani awali Zamalek wameibuka mabingwa mara 5 nao Ahly wakashinda mara 8 wakati Ismaily ikishinda kombe moja.
Ahly wameshinda kombe la ligi ya mabingwa mwaka 1982 ,1987,2001,2005,2006,2008,2012 na 2013 na kupoteza fainali mara 4 ,ya mwisho ikiwa mwaka 2018.
Zamalek wametawazwa mabingwa miaka ya 1984 ,1986 ,1993,1996 na 2002 na kushindwa katika fainali mara mbili ya mwisho ikiwa 1996.
Fainali hiyo kati ya Al Ahly na Zamalek itapeperushwa mbashara kupitia KBC Channel one kuanzia saa nne usiku