Agizo la kusitishwa kwa shughuli katika kaunti lafutiliwa mbali

Mwenyekiti wa baraza la magavana Wycliffe Oparanya ameondolea mbali lile agizo la kusitishwa kwa shughuli kwenye maeneo ya kaunti.

Akiongea wakati wa hotuba ya gavana wa Bungoma katika bustani ya chuo kikuu cha Kibabi, Oparanya alisema agizo hilo limeondolewa baada ya bunge la seneti kuafikiana kuhusu mfumo wa ugavi wa mapato kwa serikali za kaunti.

Oparanya alimshukuru rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga kwa hatua yao ya kuingilia kati na kusaidia katika utatuzi wa mzozo huo.

Akiongea,waziri wa ugatuzi Eugene Wamalwa aliyehudhuria halfa hiyo pia alimpongeza Rais kwa kuahidi kuongeza shilingi bilioni 50 kwa mgao wa fedha za kaunti mwaka ujao,akisema hatua hiyo itachangia pakubwa kudumisha ugatuzi nchini.

Pia alitoa wito wa ungwaji mikono mchakato wa BBI unaopendekeza fedha zaidi kutengewa serikali za kaunti.

Baraza la magavana lilikuwa limetangaza kusitishwa kwa huduma zinazotolewa na serikali za kaunti kutokana na uhaba wa kifedha uliosababishwa na mzozo kwenye seneti kuhusu mfumo wa ugavi wa mapato.      

Bunge la Senate lilikuwa limeshindwa mara 10 kupiga kura kuhusu mfumo wa mtu mmoja shilingi moja kura moja.

Bunge hilo lilipiga kura hiyo Alhamisi alasiri  huku maseneta wote waliochaguliwa waliokuwa bungeni wakiunga mkono.

Kamati ya wanachama 12 iliyopewa jukumu la kuleta maafikiano kuhusu mfumo huo uliokuwa ukizua utata ilikuwa imeafikia makubaliano awali.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *