Categories
Habari

Afueni kwa wakazi wa Bamba, Kaunti ya Kilifi baada ya mradi wa maji wa shilingi milioni 100 kuzinduliwa

Muungano wa Ulaya (EU) umetoa ruzuku ya shilingi bilioni 6.5 kwa hazina ya sekta ya maji kufadhili miradi ya maji kote nchini, ukiwemo ule wa Bamba-Shingaro katika Eneo Bunge la Ganze.

Afisa Mkuu Mtendaji wa hazina hiyo Ismail Fahmy Shaiye amesema pesa hizo zitasambazwa kwa kampuni zote zilizo na jukumu la kutekeleza miradi ya maji humu nchini hususan katika maeneo ya mashambani ambayo hukumbwa na ukosefu wa maji wa mara kwa mara.

Akiongea katika Wadi ya Bamba, Eneo Bunge la Ganze ambapo Gavana wa Kaunti ya Kilifi Amason Jeffa Kingi alizindua rasmi mradi wa maji kutoka Bamba hadu Shingaro utakaogharimu shilingi milioni 100, Shaiye amesema miradi hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano na serikali za kaunti.

Kulingana na makubaliano, hazina ya sekta ya maji itagharimia asilimia 87 ya fedha zinazohitajika kutekeleza miradi hiyo huku serikali za kaunti zikiongezea kiasi kilichosalia cha asilimia 13.

Katika Kaunti ya Kilifi, miradi hiyo ni Bamba-Shingaro wa shilingi milioni 100 katika Eneo Bunge la Ganze unaosimamiwa na Kampuni ya maji ya Kilifi/Mariakani (KIMAWASCO) na ule wa Kadzanani-Marereni wa shilingi milioni 45 katika Eneo Bunge la Magarini unaosimamiwa na kampuni ya maji ya Malindi (MAWASCO).

Akizungumza na waandishi wa habari katika Zahanati ya Rima ra Pera baada ya kuzindua mradi wa Bamba-Shingaro, Gavana Kingi alishukuru EU kwa ruzuku hiyo, akisema mradi huo utasaidia kukabiliana na tatizo la uhaba wa maji lililokithiri katika eneo hilo.

Amesema mradi huo pia unajumuisha ujenzi wa vituo kadhaa vya maji katika sehemu mbali mbali unapopitia mradi huo ili kuwezesha wakazi kupata huduma ya maji safi bila kutembea mwendo mrefu.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Waziri wa Maji katika kaunti hiyo Karisa Kiringi Mwachitu na Afisa Mkuu wa Idara ya Maji Kenneth Charo Kazungu, ambao wamehoji kwamba mradi huo ni afueni kwa wakazi ambao wameteseka kwa miaka mingi kwa ukosefu wa maji safi.

Wakazi wa Bamba waliozungumza na waandishi wa habari wameusifu mradi huo wa Bamba-Shingaro kuwa mkombozi wa eneo hilo kwani utawapa pumziko la kuhangaika kutafuta maji kwenye mabwawa ambayo mara kwa mara hukauka wakati wa kiangazi,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *