Afueni kwa Trump baada ya Bunge la Seneti kupungukiwa na kura za kumshitaki

Bunge la Seneti la Marekani limekosa kufikisha thuluthi mbili ya kura ili kumshitaki aliyekuwa rais wa taifa hilo Donald Trump kwa kosa la kuchochea uvamizi wa majengo ya bunge ya Capitol tarehe 6 mwezi Januari.

Maseneta 57 walipiga kura ya kumshitaki Trump, wakiwemo saba wa chama cha Republican, huku 43 wakipinga hoja hiyo.

Kura hiyo ilikosa uungwaji mkono wa maseneta 10 kufikisha angalau kura 67 zilizohitajika kumshitaki Trump.

Baada ya kuondolewa  kesi hiyo, Trump alitoa taarifa akishutumu jaribio hilo, akisema ni jaribio baya zaidi la kutaka kumpata na makosa kiongozi wa taifa katika historia ya taifa hilo.

Hii ilikuwa mara ya pili ya jaribio la kumshitaki Trump.

Iwapo angeshitakiwa, basi hangeweza tena kuwania wadhifa wowote katika Bunge la taifa hilo.

Baada ya kura hiyo, seneta mwandamizi wa bunge la Seneti wa chama cha Republican Mitch MacConnel alisema Trump alichochea uvamizi wa bunge na wafuasi wake na kukitaja kitendo hicho kuwa cha fedheha na utepetevu wa majukumu.

Awali, alipiga kura kupinga kesi hiyo akiitaja kuwa ukiukaji wa katiba kwa kua sasa Trump si kiongozi wa taifa hilo.

Hata hivyo alisema bado Trump anaweza kuwajibishwa na mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *