Afisa wa Polisi auawa kwa kupigwa risasi baada ya kumuuwa afisa mwenza

Afisa wa polisi mwenye utovu wa maadili ameuawa kwa kupigwa risasi baada ya kumuuwa afisa mwenzake kwenye makabiliano katika eneo la Kamukunji, Jijini Nairobi.

Afisa mwingine wa polisi alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya mkononi wakati wa mtafaruku huo wa usiku wa kuamkia Jumapili.

Muathiriwa wa kwanza alikuwa Konstebo Maureen Achieng, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi ndani ya gari la polisi wakati yeye na wenzake walipokuwa wakijiandaa kwenda kwa doria za usiku.

Polisi na watu walioshuhudia kisa hicho wanasema Konstebo Lawrence Ewoi alianza kugombana na Achieng kwa sababu zisizojulikana nje ya kituo hicho cha polisi.

Ugomvi huo uliendelea kwa muda mfupi kabla ya Ewoi aliyekuwa amejihami kwa bunduki kumfyatulia mwenzake risasi nne akiwa ameketi kwenye gari la polisi.

Risasi hizo pia zilimjeruhi Konstebo George Gitonga kwenye mkono wa kushoto na akapelekwa hospitalini.

Polisi wanasema Achieng alithibitishwa kuaga dunia alipofikishwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, naye Gitonga akalazwa katika hospitali hiyo.

Ewoi alitoroka lakini polisi wakaanzisha msako mkubwa wa kumtafuta.

Saa moja baadaye walimfumania na kumuua kwa kumpiga risasi karibu na Soko la Burma.

Mkuu wa Polisi katika eneo la Nairobi, Rashid Yakub, amesema kilichosababisha shambulizi la kwanza hakijabainika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *