Afisa wa Polisi akamatwa Gigiri baada ya kumuua rafikiye kwa kumtandika risasi kumi

Afisa mmoja wa polisi amekamatwa baada ya kumuua rafikiye kwa kumpiga risasi walipogombana katika eneo la Gigiri, Jijini Nairobi.

Afisa huyo wa cheo cha Konstebo anayehudumu katika Kituo kidogo cha Polisi cha Nyari, eneo la Gigiri, anazuiliwa kufuatia mauaji hayo ya usiku wa kuamkia leo dhidi ya rafikiye.

Edgar Mokamba alitumia bunduki yake aina ya AK 47 kumpiga risasi kumi rafikiye ambaye alikuwa kwenye gari lake lililokuwa limeegeshwa katika kituo hicho cha polisi baada ya ugomvi kati ya wawili hao.

Wakati maafisa wengine wa polisi walipofika mahali pa tukio hilo, walipata mwili wa mwathiriwa kwenye kiti cha dereva.

Walioshuhudia kisa hicho wanasema afisa huyo ambaye alikuwa akitafuna miraa na marehemu alipokonywa bunduki hiyo mara moja.

Afisa Mkuu wa Polisi Kaunti ya Nairobi Rashid Yakub amesema makachero wanachunguza kisa hicho ili kubaini lengo la mauaji hayo.

Mwathiriwa alikuwa mgeni wa mara kwa mara katika kituo hicho cha polisi lakini haikubainika iwapo alikuwa mpasha habari kwa polisi au rafiki tu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *