Afisa wa KDF akamatwa kwa madai ya utekaji nyara Kasarani

Watu wanne, akiwemo afisa mmoja wa Vikosi vya Ulinzi nchini KDF, wamekamatwa kwa madai ya kumteka nyara mwanaume moja katika eneo la Kasarani, Nairobi.

Kulingana na maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa maswala ya Jinai, DCI, afisa huyo wa KDF, mwenye umri wa miaka 28, na wenzake watatu walimteka nyara mwanaume huyo na kutoka nyumbani kwake hadi mahali pasipojulikana.

“Wanne hao wamekamatwa kufuatia kisa ambapo mwanaume mwenye umri wa miaka 24 alitekwa nyara kutoka nyumbani kwake na kupelekwa mahali pasipojulikana,” wamesema maafisa wa DCI.

Maafisa wa upelelezi walipopewa ripoti hiyo na jamaa wa mwanaume huyo, walianzisha uchunguzi mara moja na wakafanikiwa kumuokoa akiwa katika nyumba moja katika eneo la Kahawa Wendani, akiwa pamoja na washukiwa wa kitendo hicho.

Gari moja aina ya Toyota Noah linalosemekana kutumika kumsafirisha muhasiriwa huyo kutoka nyumbani kwake lilipatikana pamoja na simu yake na vitu vyenginevyo.

Washukiwa hao kwa sasa wamezuiliwa huku uchunguzi zaidi ukiendelea kuhusiana na kisa hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *