Categories
Kimataifa

Addis Ababa yashtumu matamshi ya Washington dhidi ya bwawa tata la Nile

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed  amesema kuwa taifa lake halita-itikia shinikizo zozote hasa baada ya rais wa Marekani  Donald Trump kupendekeza kuwa huenda Misri ikaharibu bwawa tata la Nile.

Bwawa hilo la the Grand Ethiopian Renaissance linazozaniwa na mataifa ya  Ethiopia, Misri na  Sudan.

Trump alisema kuwa Misri huenda isiweze kuishi na bwawa hilo na huenda ikalilipua.

Hata hivyo Ethiopia inaamini kuwa Marekani inaiunga mkono Misri katika mzozo huo.

Marekani ilitangaza mwezi Septemba kuwa itakatiza misaada kwa  Ethiopia baada yake kuanza kujaza eneo moja lililo nyuma ya bwawa hilo mwezi Julai.

Misri inategemea zaidi  mto Nile kwa mahitaji yake mengi ya maji na inahofia kuwa huenda huduma hizi zikakatizwa na uchumi wake kuathirika iwapo  Ethiopia itatwaa udhibiti wa mto huo.

Pindi baada ya kukamilika, bwawa hilo la gharama ya dola bilioni 4 katika eneo la  Blue Nile magharibi mwa Ethiopia litakuwa mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha kawi kutoka kwa maji barani Afrika.

Ujenzi wa bwawa hilo ulianza mwaka 2011 huku kitendawili kikuu kikiwa muda utakaotumiwa kujaza bwawa hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *