Categories
Uncategorised

Mwakilishi wodi ya Karen ahukumiwa miaka mitatu gerezani kutokana na ufisadi

Mwanachama mmoja wa bunge la kaunti ya  Nairobi amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kupokea hongo ya shilingi laki mbili.  

David Mberia ambaye ni mwakilishi wa wodi ya Karen hata hivyo alipewa fursa ya kulipa faini ya shilingi laki saba na hakimu wa mahakama ya kupambana na ufisadi ya Nairobi Thomas Nzioka.

Mberia anakabiliwa na hatari ya kufurushwa afisini hasa baada ya hakimu huyo kuagiza kuwa hastahili kuhudumu katika afisi ya umma.

Hakimu huyo aliagiza mahakama kuwasilisha nakala ya hukumu hiyo kwa spika wa bunge la kaunti ya  Nairobi ili hatua kuchukuliwa.

Mberia anadaiwa kupokea hongo kutoka kwa mfanyibiashara mmoja ili kupendelea upande mmoja katika uchunguzi unaofanywa na kamati ya bunge la kaunti hiyo kuhusu umiliki wa kipande kimoja cha ardhi kinachosemekana kumilikiwa na shule moja.

Watu wengine alioshtakiwa nao waliondolewa mashtaka.

Categories
Habari

KRA yaboresha mfumo wake wa ukusanyaji ushuru

Halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini, imezindua kampeni ya kuimarisha ulipaji ushuru kwa kuzindua mpango wa ulipaji ushuru kwa hiari-VTDP.

Mpango huo unatoa jukwaa kwa mlipa ushuru kufichua ushuru ambao hajalipa na ambao hapo awali haukuwa umefahamishwa kamishna wa ushuru kwa minajili ya kupunguziwa adhabu na riba ya ushuru huo.

Mpango huu unadhamiriwa kuimarisha ulipaji ushuru kupitia uzingativu wa zoezi hilo.

Akiongea jijini Nairobi baada ya uzinduzi wa mpango huo, kamishna wa halmashauri ya KRA wa ulipaji ushuru wa humu nchini, Rispah Simiyu, aliwahimiza walipaji ushuru kutumia vyema fursa ya kuzinduliwa mpango huo.

Alisema mara ufichuzi kamili wa ushuru ambao haujalipwa utafanywa na ushuru usio na riba kulipwa, walipa ushuru kama hao watafurahia kuondolewa riba na adhabu za ushuru ambao ulikuwa haujalipwa.

Alisema serikali kupitia halmashauri ya KRA imeanzisha mikakati kabambe za kuimarisha ukusanyaji ushuru na kukabilaiana na athari za janga la COVID-19.

Categories
Michezo

Stars kucheza mechi tatu za kujipiga msasa kabla ya kuikabili Misri

Timu ya taifa Harambee Stars imeratibiwa kucheza mechi tatu za kirafiki kunoa makali kabla ya kukabiliana na Misri katika pambo la kundi G kufuzu dimba la Afcon tarehe 22 mwezi ujao katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Stars watapambana na Sudan Kusini tarehe 13 mwezi ujao hapa Nairobi ,kabla ya kuwaalika Tanzania siku mbili baadae na kuzuru Tanzania tarehe 18 .

Kenya itawaalika Pharoes ya Misri katika pambano la tano kundi G Machi 22 kabla ya kusafiri kwenda Lome Togo kwa mkwangurano wa mwisho tarehe 30 mwezi ujao.

Mechi hizo zitakuwa za kuhitimisha tu ratiba kwa Kenya ambayo haina fursa ya kuzipiku Misri na Comoros zilizo kileleni pa kundi hilo, ili kufuzu kwenda AFCON kwa mara ya pili mtawalia kwa mara ya kwanza ,baada ya kushiriki mwaka 2019 nchini Misri.

Comoros inaongoza kund F kwa pointi 8 sawia na Misri huku timu hizo mbili zikimenyana katika mchuano wa mwisho tarehe 30 mjini Cairo Misri ,mataifa yote yakihitaji kwenda sare ili kutwaa nafasi hizo mbili.

Kabla ya hapo Comoros watakuwa na fursa ya kufuzu watakapowaalika Togo tarehe 22 mwezi Machi wakiwania tu sare ili kujikatia tiketi kwa mara ya kwanza.

Kenya ni ya tatu kundini G kwa alama 3 wakati Togo ikiwa imezoa pointi 1.

Wakati uo huo wachezaji 28 wa humu nchini wameitwa kambini kujiandaa kwa mtihani huo.

Categories
Habari

Watu 277 zaidi waambukizwa Covid-19 hapa nchini

Watu wanane zaidi wamefariki kutokana na makali ya virusi vya Covid-19 hapa nchini katika muda wa saa 24 zilizopita na kufikisha idadi jumla ya maafa kutokana na virusi hivyo humu nchini kuwa1,847.

Hayo yanajiri huku watu wengine 277 wakiambukizwa Covid-19 hapa nchini baada ya kupimwa kwa sampuli 4,599 katika muda wa saa 24 zilizopita.

Idadi jumla ya visa vilivyothibitishwa vya covid-19 hapa nchini tangu mwezi Machi mwaka jana ni 105,057 kutoka kwa idadi jumla ya sampuli 1,282,799 zilizofanyiwa uchunguzi.

Kati ya visa hivyo vipya 277 vilivyonakiliwa, 221 ni raia wa Kenya huku 56 wakiwa raia wa kigeni. Watu 173 ni wa kiume nao 104 wakiwa wa kike huku mchanga zaidi akiwa mtoto wa umri wa miaka mitatu na mkongwe zaidi akiwa na umri wa miaka 89.

Wagonjwa 336 wamelazwa katika vituo mbali mbali vya afya kote nchini huku wengine 1,397 wakiuguzwa nyumbani.

Wagonjwa 61 wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ICU, 25 kati yao wakitumia vipumulio na 27 wakipokea hewa ya ziada ya oxygen nao wagonjwa 9 wangali wanachunguzwa.

Hata hivyo wagonjwa 119 wamepona virusi hivyo vya Corona, 79 kutoka mpango wa utunzi wa wagonjwa nyumbani na 40 waliruhusiwa kuondoka katika vituo mbali mbali vya afya. Idadi jumla ya walipona ugonjwa wa Covid-19 hapan nchini sasa ni 86,497.

Kaunti ya Nairobi ingali inaongoza katika visa vipya huku ikinakili visa 194. Nakuru ilifuata kwa visa 18, Kiambu 17,Mombasa 11, Laikipia 8, Kajiado 7, Machakos 6 na Uasin Gishu visa 5.

Kaunti ya Siaya na Makueni zilinakili visa 2 kila kaunti huku Meru, Nandi, Narok, Nyandarua, Nyeri, Taita Taveta na Kisumu zikinakili kisa kimoja kila kaunti.

Categories
Michezo

Vipusa wa KCB walenga matokeo bora ligi kuu KVF Wikendi hii

Timu ya akina dada ya voliboli ya Kenya Commercial Bank inaangazia kusajili matokeo mazuri katika mzunguko wa pili wa mechi za ligi kuu KVF wikendi hii katika ukumbi wa uwanja wa Nyayo.

Timu hiyo inaendeleza mazoezi katika ukumbi wa Nyayo kujitayatisha kwa mechi hizo mbili Jumamosi na Jumapili hii.

Wahifadhi hela KCB watafungua ratiba Jumamosi dhidi ya KDF inayozidi kuimarika kabla ya kukabana koo na Kenya Pipeline siku ya Jumapili.

Kwa mjibu wa kocha mkuu wa KCB Japheth Munala watalenga kuboresha matokeo ya mechi yao dhidi ya Prison katika mkondo wa kwanza.

“Katika mechi ya mwisho dhidi ya Prisons tulipoteza kutokana na makosa tuliyofanya ,tumekaa chini na tukarekebisha makosa hayo,tutakutana na timu mbili ngumu wikendi hii na tumejitayarisha vyema na tunajiamini tutapata ushindi”akasema Munala

Timu hiyo pia imetangaza kutokuwa na majeruhi mengi,ila machache tu wanapoelekea kwa michuano ya wikendi, huku wachezaji wote wakitarajiwa kucheza.

Upande wake nahodha wa klabu hiyo Norah Murambi ,amesema wako tayari kukabiliana na timu za KDF na Pipeline mwishoni mwa juma.

“Tumefanya mazoezi kwa bidii na kubadilisha makosa tuliyofanya katika mchuano wetu wa mwisho ,timu iko katika hali shwari na tayari kwa pambano lijalo”akasema Murambi.

Categories
Burudani

Nandy na Billnass wameachana

Wanamuziki Nandy na Billnass wametengana baada ya uhusiano wa kimapenzi wa muda mrefu. Mara ya kwanza kwa watu kukisia kwamba mambo sio mazuri, ni wakati Nandy alijitokeza kutangaza kwamba pete ya uchumba aliyovishwa na Billnass ilikuwa imepotea.

Wengi walihisi kwamba Nandy alivua pete hiyo mwenyewe lakini amekuwa akijitetea akisema kwamba alivuliwa na mashabiki bila kujua kipindi cha kutumbuiza kwenye mikutano ya Kampeni mwaka jana.

Mara nyingine ni wakati alikwenda kumlaki mwanamuziki Koffi Olomide kwenye uwanja wa ndege yapata mwezi mmoja uliopita na alikuwa amemwalika kwa ajili ya kufanya kibao naye.

Nandy hakuwa na Billnass jinsi wengi walitarajia lakini Nandy alisema kwamba mpenzi huyo wake alikuwa naye kwenye mipango yote hata ingawa hakuonekana huko kwenye uwanja wa ndege.

Baadaye Nandy na Koffi walitumbuiza tena kwenye tamasha lililokuwa limeandaliwa na Clouds Media kwa ajili ya siku ya wapendanao lakini Billnass hakuonekana huko. Mamake Nandy alipohojiwa siku hiyo alisema mambo kati ya wanawe yalikuwa sawa na alikuwa anasubiri tu wampe siku ya arusi.

Billnass na Nandy

Siku ya kuzindua kibao chake na Koffi kwa jina “Leo Leo” kwenye kipindi cha “Leo Tena” cha Clouds Tv Billnass pia hakuonekana na Nandy aliendelea tu kumtetea akisema anamuunga mkono kwa kazi yake.

Nandy mwenyewe alitangaza utengano wake na Billnass wakati alikuwa anajibu shabiki mmoja ambaye alimwita mke wa Billnass kwenye picha aliyopachika kwenye Instagram.

Shabiki huyo kwa jina carinamarapachi aliandika “Mrs Billnass love uu more” naye Nandy akamjibu “Single”.

Categories
Habari

Githu Muigai apata wadhifa mpya

Aliyekuwa mwanasheria mkuu, Githu Muigai ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya pamoja ya wadau wa sekta za umma na kibinafsi.

Kwenye arifa yake katika gazeti rasmi la serikai, waziri wa fedha Ukur Yatani, alisema Muigai atakuwa mwenyekiti ilihali Mohamed Abbey Mohamed, Janice Kotut, Eunice Lumalla na Sadick Mustapha ni wanachama wa kamati hiyo.

Kamati hiyo ya pamoja ya wadau wa sekta za umma na kibinafsi,ilibuniwa chini ya kifungu cha 8 cha sheria ya ushirikiano wa sekta za umma na binafsi ya mwaka-2013 kuwa kitengo maalum kwenye wizara ya fedha.

Madhumuni ya kamati hiyo ni kutathmini na kuidhinisha miradi humu nchini.

Muigai aliteuliwa kuwa mkuu wa sheria baada ya kuratibishwa kwa katiba ya mwaka-2010.

Alijiuzulu kutoka wadhifa huo mwaka-2018 baada ya kudumu kwa kipindi cha miaka sita na nusu.

Categories
Michezo

Musa Otieno ana imani ya Kenya kufuzu AFCON 2022

Aliyekuwa nahodha wa muda mrefu zaidi wa Harambee Stars Musa Otieno ana imani kuwa timu hiyo itashinda mechi mbili za kufuzu za mwezi ujao na kujikatia tiketi kwa kipute cha AFCON mwaka ujao nchini Cameroon.

Otieno ambaye ni mmoja wa washauri wa kiufundi wa FKF amesema ana imani na mbinu za ukufunzi za kocha Jacob Ghost Mulee baada ya kuiongoza timu hiyo katika makala ya mwaka 2004 nchini Tunisia akiwa nahodha.

“Katika soka kila kitu kinawezekana,nina imani na kocha Mulee,cha mhimu ni kujiamini na kupata matokeo katika mechi dhidi ya Misri hapa Nairobi na pia tushinde Togo ugenini “akasema Otieno

Kenya ni ya tatu katika G la kufuzu kwa pointi 3 wakati Comoros na Misri zikiaongoza kwa alama 8 kila moja na ili kujikatia tiketi kwenda Afcon kwa mara ya pili mtawalia Harambee Stars hawana budi kushinda mechi zote mbili zilizosalia dhidi ya Misri Machi 22 mwaka huu uwanjani Kasarani ,na kuilaza Togo tarehe 30 mwezi ujao na kutarajia kuwa Misri na Togo hawatazoa hata pointi moja katika mechi zao mbili zilizosalia.

Otieno amelitaka shirikisho la FKF kuweka mikakati ifaayo kuanzia kwa mashindano ya shule za sekondari kuhakikisha kuwa Harambee Stars inafuzu kwa fainali za kombe la dunia mwaka ujao nchini Qatar.

“majirani zetu wametilia maanani mashindano ya shule za sekondari na pia FKF inapaswa kuyazingatia mashindano hayo na tutengeze timu thabiti za chipukizi,cha mhimu pia ni benchi ya ukufunzi kuhakikisha Kenya inashinda mechi zote za nyumbani na kutafuta sare kadhaa ugenini au hata ushindi ili kufuzu”akaongeza Otieno

Kenya imejumuishwa kundi E la kufuzu kwenda Qatar pamoja na miamba Mali,Uganda na Rwanda huku mechi hizo zikianza mweiz Juni mwaka huu ambapo timu bora kutoka kundi hilo itatinga hatua ya mwondoano.

Categories
Burudani

Firirinda Weekend!

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kuorodhesha filamu nchini Kenya KFCB Daktari Ezekiel Mutua ametangaza Wikendi inayoanza kesho kuwa wikendi ya Firirinda.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook Dakta Mutua aliandika, “Nimetangaza wikendi ijayo kuanzia kesho Ijumaa hadi Jumapili kuwa wikendi ya Firirinda kwa heshima yake na kwa ajili ya kusaidia mwandishi na mwimbaji wa wimbo huo ambaye anaugua Mzee Dickson Munyonyi. Wapiga muziki kwenye hafla zote za wikendi hii wanaombwa wacheze wimbo huo na kuhimiza mashabiki wao kuchanga fedha za kusaidia kulipa ada ya hospitali ya mwanamuziki huyo mkongwe ambaye anaendelea kupokea matibabu. Nambari ya kutuma fedha hizo kwa njia ya simu itatangazwa baada ya sisi kuwasiliana na familia na mimi nitaanzisha mchango kwa shilingi laki moja. Tuujulikanishe wimbo huu lakini zaidi na la maana ni kuutumia kusaidia mwimbaji wake ambaye anatupa kumbukumbu huku tukisherehekea utamaduni wetu.”

Dakta Mutua anasema changamoto ya Firirinda kwenye mitandao ya kijamii inafaa kuchukua mahala pa ile ya Jerusalema!

Alitumia nafasi hiyo pia kuomba yeyote ambaye anafahamu familia ya mzee huyo awasiliane naye ili amuunganishe nayo.

Kulingana na Mutua, Firirinda ni neno ambalo linatokana na maneno mawili Free la kiingereza na Rinda la kiswahili kuashiria vazi la kike.

Categories
Michezo

Brigid Kosgei ateuliwa kuwania tuzo ya 22 Laureus

Bingwa mtetezi wa London Marathon Brigid Kosgei ndiye mkenya pekee aliyeteuliwa katika orodha ya wanariadha wanaowania tuzo ya mwanamichezo bora mwaka uliopita kwenye makala ya 22 ya tuzo hiyo.

Kosgei aliye na umri wa miaka 26 alihifadhi taji ya mbio za Londona marathon mwaka uliopita ,kando na kuibuka wa pili katika mbio za Ras Al Khaima half marathon.

Kogsei anawania kuwa Mkenya wa pili kushinda tuzo hiyo baada ya Vivian Cheruiyot aliyetawazwa mshindi mwaka 2012.

Wapinzani wa Brigid kwa tuzo hiyo ni pamoja na mwendeshaji baiskeli Anna van der Breggen (Netherlands) Cycling – won both road race and time trial at World Championships kutoka Uholanzi ,Federica Brignone kutoka Italia katika mchezo wa Skiing ,bingwa wa mashindano ya Tennis ya US Open mwaka uliopita Naomi Osaka wa Japan Tennis ,nahodha wa klabu ya Lyon ya Ufaransa Wendie Renard na Breanna Stewart wa Marekani katika mpira kikapu.

Waaniaji tuzo hiyo kwa wanaume ni pamoja na Joshua Cheptegei wa Uganda aliyevunja rekodi za dunia za mita 5,000 na 10,000,Armand Duplantis wa Sweeden ,
Lewis Hamilton wa Uingereza katika mbio za langalanga ,LeBron James wa Marekani katika Basketball ,mshambulizi wa Bayern Munich Robert Lewandowskikutoka Poland
na Rafael Nadal katika Tennis akitoka Uhispania.

Shirika la Boxgirls la Kenya pia limetaeuliwa kuwania tuzo ya Laureus Sport for Good Award kutokana na juhudi za kutoa mafunzo ya masumbwi kwa jamii za mitaa ya mabanda mjini Nairobi.