Watu watano wafariki katika ajali ya barabarani Makueni

Watu watano wa familia moja waliaga dunia Jumapili jioni kufuatia ajali ya barabarani katika eneo la Kwa Ngolova karibu na kituo cha biashara cha Kivani kwenye barabara ya   Machakos-Wote katika kaunti ya Makueni.

Watu wengine watatu walijeruhiwa vibaya baada ya dereva wa gari waliloabiri kushindiwa kulithibiti na likapoteza mwelekeo kabla ya gari hilo kubingiria mara kadhaa na kuwauawa watano hao papo hapo.

Akithibitisha kisa hicho kilichotokea mwendo wa saa kumi na mbili jioni, kamanda wa polisi kwenye kaunti hiyo Joseph Ole Naipeyan alisema miongoni mwa watu walioaga dunia ni pamoja na mwanamke mmoja na watoto wake wawili,shemeji wake na mkewe.

Ole Naipeyan alisema familia hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka kwa sherehe ya kifamilia huko Mukuyuni katika kaunti ndogo ya Kaiti na walikuwa wakirejea nyumbani kwenye kaunti ya Murang’a  wakati ambapo ajali hiyo ilitokea.

Majeruhi walikimbizwa kwenye hospitali ya   Machakos Level Five huku miili ya waliofariki ikipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya kaunti ndogo ya Mukuyuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *