Yoweri Museveni kusalia mamlakani hadi mwaka-2031

Rais Yoweri Museveni wa Uganda huenda akasalia mamlakani hadi mwaka-2031 baada ya wabunge nchini humo kuidhinisha mswada tata kuhusu umri. Wabunge hao waliondoa kipengele cha katiba kinachomzuia raia ambaye hajatimu umri wa miaka-35 ama yule aliye na umri wa zaidi ya miaKa-75 kushikilia wadhifa wa urais. Yoweri Museveni ambaye ni mshirika wa karibu wa Marekani alichukua uongozi mwaka-1986 na kutokana na umri wake wa miaka-72 sasa hangeruhusiwa kuwania urais mwaka-2021. Chama tawala nchini Uganda ambacho kina wabunge wengi kilidai kuwa kipengele hicho cha katiba kuhusu umri kinabagua wakongwe. Hata hivyo mswada huo ulipingwa na wabunge wa upinzani waliovalia tepe nyekundu wakisema hatua hiyo ni sehemu ya njama ya rais Museveni kuitawala nchi hiyo hadi atakapofariki. Sheria hiyo mpya imependekeza hatamu mbili za urais kuanzia mwaka-2021. Museveni ni kiongozi wa hivi punde barani Afrika kujaribu kurefusha utawala wake kwa kubadili katiba. Hata hivyo hatua hiyo imewakera mno raia wa Uganda.