Yoweri Museveni afanya ziara rasmi nchini Kenya

Rais Uhuru Kenyatta jana alikuwa mwenyeji wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda, anayefanya ziara rasmi humu nchini. Hii ilikuwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa taifa la kigeni hapa nchini Kenya tangu kuapishwa kwa Rais Kenyatta kwa muhula wake wa pili na wa mwisho wa miaka mitano mwezi uliopita. Viongozi hao wawili walikuwa na mazungumzo ya kirafiki yaliyohudhuriwa pia na Naibu wa Rais William Ruto. Ma-Rais Kenyatta na Museveni walipongeza uhusiano mwema ulioko baina ya nchi hizi mbili, na kuahidi kwamba watajitahidi kuboresha hata zaidi uhusiano huo. Pia waliangazia maswala ya umuhimu kwa nchi zote mbili na pia kanda hii ya Afrika, ikiwa ni pamoja na hatua zilizopigwa katika ujenzi wa njia ya reli ya kisasa,(SGR) mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi (EPA) na mataifa ya Jumuiya ya Ulaya, usimamizi wa makao makuu ya jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki (EAC), vikosi vya kanda hii vya kulinda amani nchini Somalia, na pia juhudi za amani huko Sudan Kusini.