Wizara ya elimu yatangaza tarehe za mihula ya shule na vyuo

Wizara ya elimu imetangaza tarehe za mihula ya shule na vyuo za mwaka 2018. Shule za chekechea na zile za msingi zinatarajiwa kufunguliwa tarehe nne mwezi Januari na kufungwa tarehe 6 mwezi Aprili. Shule za sekondari zitafunguliwa tarehe 2 mwezi ujao huku mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne ukitarajiwa kuanza tarehe 5 mwezi Novemba. Haya yamejiri huku walimu wakuu wakiendelea kupokea barua za uhamisho ambazo chama cha kitaifa cha walimu, KNUT, kimesema kitazipinga. Walimu wakuu wa shule ya upili ya Maranda, ile ya wavulana ya Vihiga na ile ya wasichana ya Cardinal Otunga ni miongoni mwa wale walioathiriwa na hatua ya kuwahamisha walimu wakuu. Mwalimu mkuu wa shule ya upili wa Maranda Boaz Owino amehamishiwa shule ya upili ya Nyambaria katika kaunti ya Nyamira. Wengine walioathiriwa ni mwalimu wakuu wa shule ya wavulana ya Musingu na mwenzake wa Chavakali Kai Indimuli ambaye amehamishiwa shule ya upili ya wavulana ya Machakos. Wengine ni mwalimu kuu wa shule ya upili ya wasichana ya Lugulu, Margaret Mechumi ambaye amehamishiwa shule ya upili ya wasichana ya Kisumu ambapo mahala pake patachukuliwa na Dinah Chebii wa shule ya upili ya wasichana ya Kapsowar ya Elgeyo Marakwet. Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Kakamega Oliver Munishi amehamishiwa Nanyuki. Uhamisho huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Januari mwaka ujao huku walimu hao wakuu wakiwa tayari wamepokea barua zao.