Wizara Ya Ardhi Yataka Bajeti Yake Iongezwe Kwa Shilingi Bilioni Mbili

Wizara ya ardhi inataka bajeti yake iongezwe kwa shilingi bilioni mbili zaidi ili kuiwezesha kutoa hati milioni moja zaidi za umiliki ardhi kabla ya mwisho wa mwaka ujao. Waziri wa ardhi, Profesa Jacob Kaimenyi, amesema wizara ya ardhi tangu mwaka wa 2013 imetoa zaidi ya hati milioni tatu za umiliki ardhi kwa Wakenya. Hata hivyo waziri alisema fedha ambazo wizara hiyo inazo kwa sasa haziwezi kutosha kugharamia utoaji hati zaidi za umiliki ardhi. Akiongea na wanahabari katika chama cha wahudumu wa benki nchini hapa jijini Nairobi jana baada ya kukutana na wafanyikazi wa wizara hiyo. Kaimenyi alisema makundi nane yamebuniwa kusimamia na kuharakisha utoaji hati za umiliki ardhi kwa miongoni mwa wengine mipango ya makazi ya maskwota na maeneo ambako ardhi haijagawanywa kote nchini. Waziri Kaimenyi pia alisema wizara ya ardhi pia itazindua zoezi la kuweka mipaka ya ardhi ili kuepusha kesi mahakamani zinazotokana na mizozo ya umiliki ardhi kwa kutumia mfumo wa gharama nafuu.