Wizara Ya Afya Kugharamia Matibabu Ya Manusura Wa Mkasa Wa Huruma

Wizara ya afya imetangaza kwamba itagharamia matibabu ya manusura wa mkasa uliotokea mtaani Huruma ambao wanapokea matibabu katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta. Akiwahutubia wanahabariA� katika hospitali hiyo baada ya kuwazuru manusura 12 ambao bado wamelazwa katika hospitali hiyo waziri wa afya Dr. Cleopa Mailu alisema kuwa wizara hiyo inashirikiana na hospitali hiyo kuhakikisha kwamba manusura hao wanapata matibabu bora.

Alisema kuwa manusura hao wanaendelea kupata nafuu na sasa wako katika hali thabiti. Kadhalika alisema kuwa manusura hao 12 wanaotibiwa watapewa usaidizi wa kiakili na kijamii kabla ya kuruhusiwa kuondoka hospitalini. Alisema kuwa wizara hiyo kwa ushirikiano na makundi ya waokoaji likiwemo shirika la msalaba mwekundu nchini na mashirika mengine ya kiserikali wamechukua hatua za kuhakikisha kwamba wale waliopoteza makazi yao wanapewa makazi ya muda. Takwimu za wizara ya afya kufikia sasa zinaonyesha kwamba idadi ya wale waliofariki imefikia watu 21 huku 65 wakiwa bado hawajulikani waliko.