Wizara ya afya imefunga hoteli 17 Kangundo kaunti ya Machakos

Wizara ya afya imefunga hoteli 17 katika kaunti ndogo ya Kangundo kwa muda usiojulikana kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu katika kaunti hiyo.A� Afisa wa afya katika kaunti ndogo ya Machakos Zachary Ochonga alisema kuwa hoteli hizo 17 hazitaruhusiwa kuendesha shughuli zake hadi pale zitakapoidhinishwa na afisi yake. Alisema kuwa hoteli hizo hazijazingatia kanuni za usafi na hivyo ni tishio kwa afya ya umma. Afisa mkuu wa afya katika kaunti ya Machakos Jackson Nthanga, jana alidhibitisha kuwa wale waliopatikana na ugonjwa wa kipindupindu wamelazwa katika hospitali ya kikatoliki ya askofu Kioko. Aliwahimiza wakazi wa eneo hilo kuzingatia viwango bora vya usafi. Wakati uo huo, wafungwawatatu katika gereza kuu la Kodiaga wamelazwa hospitalini baada ya kuonekana kuwa na dalili za ugonjwa wa kipindupindu. Kulingana na naibu kamishna wa gereza hilo Martin Akwanyi, mmoja wa wafungwa hao alizuiliwa katika zahanati ya gereza hilo baada ya kuanza kuhara huku wengine wawili wakipata matibabu katika zahanati hiyo. Alisema kuwa sampuli zilizopelekwa katika taasisi ya utafiti wa kimatibabu ya Kenya a��KEMRI- zilithibitisha kuwa mmoja wa wafungwa hao alikuwa na kipindupindu. Alisema kuwa tayari wamewafahamisha maafisa wa afya ya umma kuhusu kisa hicho. Wakenya wamehimizwa kuzingatia viwango vya juu vya usafi na kutumia maji yaliyotibiwa kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu.A� Kufikia sasa kaunti 12 zimeripotiwa kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu huku kaunti za Nairobi na Garissa zikiathirika zaidi.