Winnie Madikizela-Mandela atazikwa tarehe 14 mwezi huu

Marehemu Winnie Madikizela-Mandela,  shujaa wa mapambano dhidi  ya uliokuwa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini   ataandaliwa mazishi ya  kitaifa tarehe 14   mwezi huu. Hiyo ni kwa mujibu wa Rais wa nchi hiyo    Cyril Ramaphosa  ambaye  alisema hayo baada ya kuzuru nyumbani kwa mwenda zake katika mtaa wa Soweto mjini  Johannesburg.   Kwenye ujumbe wa rambirambi uliotangazwa katika televisheni, Rais Cyril Ramaphosa alisema  mwenda zake  alikuwa  mpiganiaji  wa  haki na usawa  ambaye   kujitolea  kwake  kukabiliana na  masaibu ya watu  kulimpa  upendo na heshima ya taifa.  Winnie ambaye alikuwa  mke wa  Rais wa kwanza mweusi wa Afrika   Kusini  kabla ya kutengena  naye   alifariki baada ya kuugua tangu mwanzoni  mwa mwaka huu.   Akijulikana kama  Nomzamo Winifred Zanyiwe Madikizela,  alizaliwa tarehe Septemba   26, 1936.  Marehemu  alijulikana pia kama  Mama Winnie  na Mama Taifa. Winnie alikuzua katika mkoa wa Cape Mashariki  na hatimaye akahamia mjini  Johannesburg kufanya kazi kama  mwanamke wa kwanza mweusi mhudumu wajamii  ambapo alikutana na Mandela mwaka 1957 akiwa wakili na mwanaharakati wa kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi aliyemzidi umri kwa miaka 18.   Walifunga ndoa baada ya Mandela kumpa talaka mkewe wa kwanza.