WHO: Virusi Vya Zika Kuenezwa Kwa Njia Ya Kujamiana

Shirika la afya duniani –WHO limesema kuwa kuna ushahidi wa kutosha kwamba virusi vya Zikas vinaenezwa sana  kupitia kujamiana kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.Ukweli huo unadhihirisha kuenea kwa  visa vya ugonjwa huo ambao unaathiri ubongo na kasoro nyingine za kimaumbile katika miili ya watoto.Baada ya mkutano wa dharura wa kamati maalum ya shirika hilo,mkurugenzi mkuu wa  WHO Margaret Chan  alisema kuwa kulingana na ripoti na uchunguzi ambao umefanywa katika mataifa tofauti  zinaonesha kuwa  virusi vya ugonjwa wa Zikas huenezwa kupitia ngono kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.Marekani imezindua uchunguzi kuhusu visa vya maambukizi ya virusi hivyo kwa njia ya kujamiana.Shirika la afya duniani limependekeza   wanawake wajawazito kutozuru nchi ambazo kumeripotiwa kutokea ugonjwa huo.Aidha limesema ikiwa wanaume wao wametembelea nchi zilizoathiriwa wajiepushe na mtindo wa kufanya ngono  kiholela au wajiepushe kabisa na mambo ya kujamiana wakati wa ujauzito.