WHO kusaidia serikali kutoa huduma za afya

Shirika la afya duniani, WHO,A�A�limeahidi kuunga mkono kikamilifu mpango wa kutoa huduma za afya kwa wote katika muda wa miaka mitano ijayo. Mkurugenzi mkuu wa shirika la WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alitoa matamshi hayo alipomtembelea rais Uhuru Kenyatta katika ikulu ya Nairobi. Tedros, ambaye yuko kwenye ziara yake ya kwanza rasmi hapa nchini akiwa mkurugenzi mkuu wa shirika la WHO, alisema shirika lake liko tayari kushirikiana na serikali kuimarisha utoaji huduma za afya na pia kuthibiti nafasi ya nchi hii kama kitovu cha huduma za afya katika kanda hii. Mkurugenzi mkuu huyo aliahidi kushirikiana na serikali katika kuwaleta wataalamu wa afya kusaidia kustawisha mfumo wa afya ambao utawezesha utoaji huduma za afya kwa Wakenya wote. Kiongozi wa nchi alisema ameratibu mpango ambao atautekeleza ili kuhakikisha Wakenya wote wanapokea huduma za afya zilizoimarishwa na za gharama nafuu. Rais Kenyatta alisisitiza haja iliyopo ya kuimarisha afya ya kimsingi, akisema anazingatia kuimarisha uwezo wa serikali za magatuzi wa kutoa huduma za afya.