Waziri Wa Maswala Ya Vijana Sicily Kariuki Awahimiza Wakenya Kutoingiza Siasa Kwenye Miradi Ya NYS

Waziri wa masuala ya vijana Sicily Kariuki amewahimiza Wakenya kukoma kuingiza siasa kwenye miradi inayotekeleza na shirika la huduma ya vijana kwa taifa akisema inalenga kuboresha maisha ya vijana hapa nchini. Akiongea wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo katika eneo bunge la Runyenjes katika kaunti ya Embu, Kariuki alisema serikali imejifunza mengi kuhusu usimamizi wa miradi hiyo baada ya miradi ya hapo awali kukumbwa na changamoto. Miradi ya hapo awali iliyochukua muda wa miezi tisa katika maeneo bunge 72 ilikumbwa na madai ya ufisadi huku maafisa wakuu wa shirika la NYS wakishutumiwa kwa ufisadi. Kariuki alisema serikali haitaruhusu watu wachache wachoyo kutumia miradi hiyo kujitafutia umaarufu wa kisiasa akisema kufikia sasa vijana wengi wamenufaika kutokana na miradi hiyo.