Waziri Wa Elimu Aahidi Kuboresha Mtaala Wa Elimu

Mtaala wa sasa wa elimu hauangazii changamoto zinazoikabili nchi hii. Hayo ni kwa mujibu wa waziri wa elimu Dkt Fred Matiangi alipokuwa akiwahutubia wanahabari kuhusu mpango wa kuangazia upya mtaala wa masomo hapa nchini. Akiongea kwenye hoteli moja jijini Nairobi leo asubuhi, waziri Matiang’i alisemaA�changamoto za kiteknologia zinazoikabili nchi hii zimepuuzwa hasa wakati huu ambapo Kenya inajikakamua kuafikia malengo ya ruwaza ya mwaka 2030 kuhusu mfumo bora wa elimu. Aliwahimiza wadau katika sekta ya elimu ikiwemo vyuo vikuu kuchangia vilivyo katika harakati hizo. Taasisi ya kubuni mitaala ya masomo hapa nchiniA� imeanzisha shughuli ya kuangazia mahitaji ambayo matokeo yake yatakuwa na mchango mkubwa katika hatua hiyo ya marekebisho. Sera ya kuangazia upya mtaala wa masomo inalenga kuwapa wakenya mtaala bora zaidi kuliko ule wa sasa ambao umechochea elimu duni shuleni. Mtaala huo mpya utasisitiza utambuzi wa mapema waA� talanta na kukukuza vipaji hivyo, mbali na kubuni amali za kitaifa za kuhimiza uwiano na utangamano.