Yahofiwa Waathiriwa Zaidi Wamenaswa Kwenye Vifusi Kisii

Jumba moja la ghorofa liliporomoka jana mjini kisii na kuwauwa watu wawili huku wengine 31 wakijeruhiwa.Inahofiwa kwamba huenda waathiriwa zaidi wamenaswa kwenye vifusi vya jumba hilo.

Majeruhi wawili wamepelekwa katika hospitali ya rufaa ya kisii kwa matibabu. Jumba hilo ambalo lipo katika maeneo ya barabara ya pembezoni ya Darajamoja-Nyamataro mjini Kisii, lilikuwa likiendelea kujengwa wakati lilipoporomoka na kulikuwa na zaidi ya wafanyakazi 30 kwenye jengo hilo wakati mkasa huo ulipotokea.

Gavana wa kaunti ya kisii James Ongwae aliyefika kwenye eneo la mkasa huo kusimamia shughuli za uokoaji alililaumu liliokuwa baraza la mji wa Kisii kwa kuidhinisha ujenzi wa jumba hilo lililokumbwa na mkasa.Hata hivyo aliwahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kwamba hospitali ya rufaa ya kisii imetoa vifaa vya kutosha kuokoa maisha.

Kamishna wa kaunti hiyo, Kula Hache amesema kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya maafisa ambao waliozembea katika kutekeleza majukumu yao,Naye gavana wa Nyamira John Nyagarama alishtushwa na tukio hilo na akaahidi kutoa mashine kutoka kaunti ya Nyamira kusaidia katika shughuli za uokoaji.