Wavuvi Wa Kaunti Ya Migori Waunda Vikundi Vya Kukabiliana Na Mabaharia Katika Ziwa Victoria

Wavuvi katika kaunti ya Migori wamebuni makundi ya kushika doria ili kukabiliana na ubaharia katika ziwa Victoria baada ya kupoteza mabilioni ya pesa kupitia samaki waliovuliwa na vifaa vya uvuvi kwa majambazi. Kulingana na msimamizi wa ufuo wa Olasi, Peter Ouma, wavuvi hao wameazimia kufadhili shughuli za kundi hilo kwa kutoa michango ya mara kwa mara. Hatua hii inafuatia madai ya polisi kushindwa kuhakikishia usalama kwa wavuvi na vifaa vyao vya uvuvi. Wale wanaoendesha shughuli zao katika ufuo huo walidai wamepoteza injini tatu za mashua za uvuvi na vifaa vingine vya thamani ya shilingi milioni nne kwa mabaharia wanaoaminika kutoka katika kaunti jirani. Hatua hii pia inajiri wakati wavuvi katika kisiwa cha Migingo wamelalamikia kuhangaishwa mara kwa mara na maafisa wa usalama wa Uganda, ambao kila mara huchukua samaki wao na vifaa vya uvuvi wakiwalaumu kwa kuvuka mpaka.