Watu Wawili Wapoteza Maisha Katika Ajali Ya Kiambu

Watu wawili walifariki leo asubuhi kwenye barabara ya Ndenderu-Limuru, kaunti ya Kiambu. Ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa lori aliposhindwa kulidhibiti baada ya hitilafu za kimitambo ambapo alipoteza mwelekeo na kugonga magari matano likiwemo basi la shule ya msingi ya Dhamana. Dereva wa lori hilo pamoja na mwanafunzi mmoja walifariki papo hapo. Waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali mbalimbali mjini huko Kiambu kabla ya baadhi yao kuhamishwa hospitali nyingine. Muuguzi mkuu katika hospitali ya Mercy Light, Wangechi Munyeki alisema walipokea wanafunzi wanne huku mmoja akiwa tayari amefariki. Wanafunzi wengine waliokuwa na majeraha vichwani na tumboni walipelekwa katika hospitali mbalimbali jijini Nairobi kwa matibabu maalum. Afisa mkuu wa polisi katika eneo la Kiambaa Stephen Ngetich alithibitisha kisa hicho na kutoa wito kwa madereva kuwa waangalifu barabarani.