Watu watatu wahofiwa kufariki kutokana na kipindipindu Kisumu

Watu watatu wanahofiwa kufariki na wengine 28 kulazwa hospitalini mjini Kisumu baada ya ugonjwa wa kipindupindu kuzuka mjini humo. Wawili kati ya wale waliofariki walikuwa kwenye gereza la Kodiaga huku wafungwa 28 wakiendeleza kupokea matibabu kwenye vituo mbalimbali vya afya katika eneo hilo. Hata hivyo Waziri wa afya Cleopa Mailu amesema visa vya maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini vimepungua pakubwa kufuatia kuimarishwa kwa harakati za kudhibiti ugonjwa huo. Kwenye taarifa, Mailu alisema visa vya ugonjwa wa kipindupindu vinavyoshuhudiwa kila siku vimepungua kutoka 60 hadi 35. Hali hiyo imetokana na mikakati kama vile ushirikiano wa wadau ambao umesaidia katika kudhibiti ugonjwa huo. Wizara ya afya inaendelea kuwakumbusha wananchi wadumishe viwango vya juu vya usafi, kupata maji ya kunywa kutoka vyanzo salama na kuweka dawa kwa maji ya matumizi ya nyumbani.