Watu Watatu Wafariki Baada Ya Ukuta Kuwaangukia Mtaani Westlands

Watu watatu wamethibitishwa kufariki huku wengine saba wakilazwa hospitalini baada ya ukuta kuwaangukia mtaani Westlands jijini Nairobi . Wale waliojeruhiwa na marehemu walikuwa wakifanya kazi ya ujenzi ambapo walikuwa wakichimba mtaro karibu na ukuta katika barabara ya Brookside drive mkasa huo ulipotokea. Miili ya marehemu imeondolewa. Eneo hilo hukumbwa na mafuriko kila kunaponyesha na wafanyikazi hao walikuwa wakichimba mtaro mkubwa kusaidia kuthibiti mtiririko wa maji. Shirika la msalaba mwekundu limesema kuwa mkasa huo ulitokea mwendo wa saa saba jana mchana wakati wafanyikazi hao walipokuwa katika kina kirefu ndani ya mtaro huo wakati kuta zilipoporomoka. Hiki ni kisa cha hivi punde zaidi kutokea katika muda wa juma moja. Mnamo tarehe 21 mwezi uliopita, wafanyikazi wanne walifariki katika eneo la Westlands katika barabara ya Peponi jijiniA� Nairobi baada ya ukuta kuporomoka. Watu tisa waliokolewa wakiwa hai na kupelekwa kwenye hospitali iliyo karibu ambapo walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka.