Watu wanane wajeruhiwa kwenye ajali ya barabarani eneo la Molo

Watu wanane walijeruhiwa leo asubuhi kwenye ajali ya barabarani iliyohusisha basi la shule katika eneo la Molo, kaunti ya Nakuru. Ajali hiyo ilitokea baada ya basi hilo la shule ya upili ya Queen of Peace, Ruriuni kugongana na gari aina ya Toyota Noah katika sehemu ya Kibunja. Waliojeruhiwa walipelekwa kwa matibabu katika hospitali ya Molo Level Four. Wakati huo huo, watu-18 walifariki jana jioni na wengine tisa kujeruhiwa baada ya matatu waliyokuwa wakisafiria kugongana na lori katika eneo la Kilimambogo kwenye barabara ya Thika-Garissa. Majeruhi walipelekwa katika hospitali ya Thika level 5 na ile ya kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu. Kulingana na walioshuhudia ajali hiyo, dereva wa matatu hiyo ya abiria-14 iliyokuwa ikisafiri kutoka Nairobi kuelekea Kitui aligonga piki piki kabla ya kugongana na lori lililokuwa likitoka upande wa pili. Abiria-11 katika matatu hiyo ya chama cha Kinatwa walifariki papo hapo huku wengine wakifariki katika hospitali hiyo ya Thika level 5. Kufikia sasa zaidi ya watu-170 wamefariki kwenye ajali za barabarani mwezi huu wa Disemba.